1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawaonya raia wake katika nchi ya Ulaya

Admin.WagnerD4 Oktoba 2010

Kufuatia kugundulika kwa njama za mashambulizi ya kigaidi katika nchi za Magharibi, Marekani yatoa onyo kwa raia wake wanaotembelea nchi za Ulaya. Onyo hili linaweza kuuathiri uchumi wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/PUIS
Maafisa wa Polisi wa Ufaransa wakiwa kwenye Mnara wa Eiffel Tower baada ya kitisho cha kuwepo kwa bomu lililotegwa kwenye eneo hilo katikati ya mwezi uliopita
Maafisa wa Polisi wa Ufaransa wakiwa kwenye Mnara wa Eiffel Tower baada ya kitisho cha kuwepo kwa bomu lililotegwa kwenye eneo hilo katikati ya mwezi uliopitaPicha: AP

Indhari hii ya serikali ya Marekani kwa raia wake wanaotembelea nchi za Ulaya, inatajwa na wachambuzi wa mambo ya usalama kwamba, siyo ile inayoitwa "onyo la kusafiri" ambayo kwa kawaida huwazuia kabisa Wamarekani kutokutembelea maeneo yanayotajwa.

Indhari ya mara hii, inawataka tu Wamarekani wanaotembelea nchi hizi za Ulaya wachukuwe tahadhari na wajilinde wenyewe, kwa mfano, wajiepushe kutembelea maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu, kama vile vituo vya usafiri wa umma na vivutio vya watalii.

Lakini baadhi ya nchi za Ulaya zimekwenda mbali zaidi ya hapo. Kwa mfano, mara tu baada ya Marekani kutangaza indhari yake, Uingereza nayo ikalihariri tamko lake la indhari kwa raia wake walioko nchi za Ufaransa na Ujerumani, kwa kusema kwamba nchi hizo "zina kitisho kikubwa cha mashambulizi ya kigaidi." Italia na Ufaransa nazo, zikakubaliana moja kwa moja na indhari ya Marekani, huku Kamisheni ya Ulaya ikasema bado inaingalia hali kabla ya kutoa tamko rasmi. Lakini Ujerumani inaona kwamba hadi sasa hakujakuwa na haja ya kubadilisha tangazo lake la indhari ya usalama kufuatia wasiwasi huo uliooneshwa na Marekani.

Vyanzo vya usalama vinasema kwamba, kama njama hizi zingelifanikiwa, basi mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, ungelikuwa miongoni mwa miji ya Ulaya ambayo ingelitikiswa na mashambulizi ya kikomandoo, kama yale yaliyolitikisa jiji la Mumbai, India, mwaka 2008, ambayo yalipoteza maisha ya watu 173.

Leo, gazeti la kila wiki la hapa Ujerumani, Der Spiegel, limeripoti kwamba mpango huu wa mashambulizi dhidi ya miji ya Ulaya ulipangwa na kiongozi namba tatu wa Al Qaeda, Sheikh Yunis al-Mauretani, akisaidiwa na Osama bin Laden. Al-Mauretani ndiye aliyemshirkisha kwenye mpango huu raia wa Ujerumani mwenye asili ya Kiafghanistan, Ahmad Siddiqui, ambaye kwa sasa anashikiliwa katika kituo cha wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan.

Pamoja na kuzimwa kwa njama hizi za mashambulizi ya kigaidi, tayari athari zake zinaweza kuonekana barani Ulaya. Sekta ya utalii ni miongoni mwa maeneo yatakayoathirika sana, kutokana na tangazo hili la indhari kwa raia wa Marekani barani humu. Tabia ya kupenda matumizi waliyonayo Wamarekani inazinufaisha sana nchi wanazotembelea. Karibu Wamarekani milioni saba waliitembelea Ulaya mwaka uliopita na kuliingizia bara hili dola bilioni 412 za Kimarekani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP


Mpitiaji: Hamidou Oummilkheir