Marekani yashambulia Afghanistan
14 Aprili 2017Bomu hilo halijawahi kutumika kabisa katika mapambano ya jeshi la Marekani , wamesema maafisa wa wizara ya ulinzi , Pentagon. Wapiganaji 36 wa kundi la Dola la Kiislamu waliuwawa katika shambulio.
Bomu hilo , linalofahamika kama GBU-43B , ama silaha kubwa kabisa ya kushambulia toka angani, lina nguvu za tani 11 za miripuko . Lilipotengenezwa katika miaka ya mwanzo ya 2000, wizara ya ulinzi Pentagon , lilifanya mapitio ya uhalali wake rasmi wa kutumika katika mapambano.
Wizara ya ulinzi ilisema haina makadirio ya vifo ama uharibifu unaoweza kusababishwa na shambulio la bomu hilo, ambalo rais wa Marekani Donald Trump ameliita lililofanikiwa kabisa. Lakini imesema katika shambulio hilo, wapiganaji 36 wa kundi la Dola la Kiislamu waliuwawa , lakini hakuna raia wa kawaida aliyeuwawa, na kuongeza kwamba mahandaki kadhaa ya IS pamoja na silaha vimeharibiwa.
Makao makuu ya jeshi la Marekani mjini Kabul yamesema katika taarifa kwamba bomu hilo lilidondoshwa majira ya saa za mchana saa za Afghanistan jana katika mfumo wa njia za chini ya ardhi zilizochimbwa na wapiganaji katika wilaya ya Achin katika jimbo la Nangarhar, ambako kundi linalohusiana na Dola la Kiislamu wamekuwa wakifanya shughuli zao.
Shambulio hilo lililenga eneo karibu na mpaka na Pakistan.Mshauri mwandamizi wa taasisi ya mikakati na mitaala ya kimataifa katika mpango wa usalama wa kimataifa, Mark F. Cancian kuhusu shambulio hilo amesema.
"Tuliona baadhi ya taarifa za habari kwamba kulikuwa na mfuko wa njia za chini ya ardhi nchini Afghanistan na Marekani ilishambulia kwa silaha maalum , kile kinachojulikana kama MOAB , bomu kubwa linaloweza kuvunja kutoka angani."
Marekani inakadiria kwamba wapiganaji 600 hadi 800 wa kundi la IS wapo nchini Afghanistan , hususan katika jimbo la Nangarhar. Marekani imekuwa ikielekeza nguvu zake nyingi katika kupambana nao wakati huo huo kuyasaidia majeshi ya Afghanistan kupambana na kundi la Taliban.
Ni wiki iliyopita tu mwanajeshi wa kikosi maalum cha jeshi la Marekani , staff sajini Mark R. De Alencar , mwenye umri wa miaka 37 akitokea Edgewood , maryland , aliuwawa katika mapambano katika jimbo la Nangarhar.
Bomu hilo la MOAB ni silaha iliyotengenezwa maalum kwa ajili ya jeshi la anga ambayo ilikuwa imehifadhiwa tu katika hazina ya silaha kwa zaidi ya muongo mmoja lakini haikutumika katika mapambano, licha ya kuwa ilikuwapo wakati wote wa vita vya Iraq.
Mark F. Cancian anaelezea kwa nini silaha hiyo imetumika hivi sasa.
"Nafikiri kuna mambo yanaendelea katika maeneo mawili. Kwanza huu ulikuwa uamuzi wa mbinu ya kijeshi. Unakuwa na lengo kama hili muhimu, njia za chini ya ardhi zilizoko katika kina kirefu na kisha una hii silaha ambayo imeundwa kwa ajili ya kushambulia maeneo maalum kama hayo, kwa hiyo nadhani kwa jeshi lilikuwa suala la eneo ambalo si la kawaida kushambulia kwa silaha maalum.
Katika mapitio yake ya mwaka 2003 kuhusiana na uhalali wa matumizi ya MOAB , wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon ilitoa hitimisho kwamba haiwezi kuitwa silaha ya maandangamizi chini ya sheria ya mapambano ya silaha.
Mwandishi: Sekione Kitojo / APE
Mhariri: Caro Robi