1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yapinga wito wa kupunguza utoaji wa gesi chafu

Siraj Kalyango10 Desemba 2007

Al Gore mshindi wa tuzo la mazingira mwaka 2007

https://p.dw.com/p/CZdX
Kutoka kushoto kuelekea kulia, rais wa tume ya Ulaya, Jose Manuel Barroso, Mshindi wa Nobel kutoka Kenya mwaka 2004 Wangari Maathai, na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na makamu rais wa zamani wa Marekani na mshindi wa Nobel mwaka 2007 Al Gore nje ya Elysee Palace mjini Paris, Alhamisi Oct. 25 , 2007Picha: AP

Mkutano kuhusu hali ya hewa unaofanyika Bali Indonesia ndio umeingia katika wiki ya pili na muhimu.

Umuhimu unatokana na kuwa huku makundi yanayotetea mazingira yakionya wajumbe wa mkutano huo kufikia muafaka kuhusu hali ya hewa ili kuufanikisha, hata hivyo Marekani kwa upande wake, imesema kamwe haitakubali mapendekezo ya mkutano huo ya kupunguza utoaji wa gesi chafu.

Mawaziri wanaohusika na mazingira wapatao 20 kutoka nchi mbalimbali duniani wanakutana leo na kesho mjini Bali kunakofanyika mkutano wa hali ya hewa. Mkutano huo umeandaliwa na Umoja wa Mataifa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa-Ban Ki-moon amezihimiza nchi zinazonukia kuchukua hatua muafaka ili kupambana dhidi ya kubadilika kwa hali ya hewa. Katibu mkuu amesema hayo mjini Bangkok Thailand akiwa njiani kuelekea Bali ambako washirikia wanajaribu kupanga mkakati mpya wa kupambana dhidi ya hewa chafu zinazosababisha kubadilika kwa mazingira.

Mawaziri wa mazingira wanasubiriwa na muswada jaribio ambao unalenga sana utoaji wa gesi chafu.Hii ikiwa ni mara ya kwanza kuona kuwa juhudi za pamoja zinafanywa ili kupunguza uchafuzi wa mazingira katika nchi zinazoendelea.

Hata hivyo Marekani kwa upande wake imesema haitatii maamuzi ya mkutano huo. Kiongozi wa ujumbe wa Marekani katika mkutano huo, Harlan Watson, nae amekataa ujumbe wa kupunguza gesi ulioko katika pendekezo litakalotolewa Ijumaa. Miongoni mwa mengine pendekezo hilo litatoa ratiba ya kufuatwa ili kuelekea kupata mkataba mwingine utakaochukua pahala pa mkataba wa Kyoto.Pendekezo linazitaka nchi zilizoendelea kupunguza kiasi cha gesi chafu zinazokitoa.Pendekezo linataka kiwango kiwe asilia mia 40 chini ya kile kilichowekwa mwaka wa 1990.Mkutano wa Bali unataka kiwango kipunguzwe kwa asili mia 25 hadi mwaka wa 2020.

Huku Marekani ikikataa kutii mapendekezo ya mkutano wa Bali kwa upande mwingine raia wake na mtu mashuhuri anapokea tuzo kwa juhudi zake kuuhamaisha ulimwengu kuhusu elimu ya hali ya hewa.Katika sherehe ya mjini Oslo, makamu rais wa zamani wa Marekani Al Gore atapokea tuzo la Nobel.

Al Gore aliuambia mkutano wa Bali kuwa kizazi hiki kisipuuze masuala ya kubadilika kwa hali ya hewa.

''…je tunataka kutambulika katika vitabu vya historia vya hapo baadae kuwa tulikuwa kizazi ambacho hakikujali na ambacho kilikuwa haribifu ambacho kilifikiria tu masuala ya mda mfupi na eti hatukujali kizazi kijacho? Mimi kamwe sikubali kuwa hatuna mwoyo wa huruma na naamini kuwa tunaweza kuzuia uharibifu huo,'' amesema Al Gore.

Na hayo yakiarifiwa ripoti moja iliotolewa katika mkutano wa Bali inasema kuwa ujoto duniani unaweza ukasababisha kuhama kusio na kifani, kuvurugika kwa biashara na pia kusababisha migogoro ya ardhi na maji kutoka bara la Afrika hadi bara la Asia.Ripoti ambayo imetolewa na baraza la ushauri kuhusu mazingira la Ujerumani, inasem akuwa mda unayoyoma kwa mataifa kukubaliana kuhusu kupunguza gesi chafu kabla ya joto halijaongezeka duniani, pamoja na kupanda kwa kima cha maziwa,theluji katika ncha za dunia kuyeyuka na pia ukame na mafuriko kuongezeka na hivyo kuzusha mtafaruko duniani.