1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani - September 11

11 Septemba 2010

Rais Barack Obama amewaomba raia kuwa na umoja, huku mpango wa kuichoma Quran tukufu ukifutilia mbali.

https://p.dw.com/p/P9uO
Jamaa za wahanga wa shambulio la Sept. 11, 2001 katika eneo la World Trade Center.Picha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama amehutubia wananchi nchini Marekani na kuweka shada la maua katika eneo ambalo ndege mojawapo iliyotekwa nyara na magaidi ililijibamiza na jengo la wizara ya ulinzi, Pentagon nje ya mji mkuu wa Washington.


 Kiongozi huyo amewakumbusha wananchi wa Marekani juu ya umoja walio nao nchini humo kufuatia kumbukumbu ya miaka 9 ya shambulio la Septemba 11 na kuwaomba wazingatie lile linalowaunganisha na sio yale yanayowatenganisha.

Gedenkfeier USA New York 11. September
Familia zilizokusanyika katika maadhimisho ya Septemba 11,katika eneo la World Trade Center,wanasikiza majina ya wahanga yakisomwa.Picha: AP

Rais Obama amesema hayo mjini Washington katika maadhimisho ambayo yanajiri kukiwa na mgongano kati ya jamii za dini tofauti nchini humo. Mpango wa kujenga msikiti katika eneo la Manhattan sio mbali na eneo la World Trade Center lilioshambuliwa na mashambulizi hayo ya kigaidi, umezua mjadala mkali nchini humo.

Pia mchungaji mwenye itikadi kali za dini ya Kikristo,Terry Jones,wa kanisa moja katika jimbo la Florida, aliyepanga kuchoma kitabu kitukufu cha dini ya Kiislamu,Quran, katika kumbukumbu ya siku hii ,amenukuliwa na vyombo vya habari mjini New York hii leo,akisema kuwa kamwe hatochoma kitabu hicho kitukufu. Jones ameliambia shirika la habari la NBC, kuwa sio leo tu, bali milele kanisa hilo halitoichoma Quran hiyo.

Aliyasema haya baada ya kuulizwa na waandishi habari iwapo kanisa lake lingeendelea na mpango huo siku nyingine.

Mpango wake huo ulilaaniwa duniani kote na kuzusha hofu ya mashambulio ya kulipiza kisasi dhidi ya vikosi vya Marekani vilioko nje.

Mwandishi: Maryam Abdalla/AFPE

Mhariri: Dahman Mohammed