1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuwahoji wake wa Osama

Halima Nyanza10 Mei 2011

Marekani inatarajia kuwa Pakistan itairuhusu katika siku za karibuni kuwahoji wake wa aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa al Qaeda, Osama bin Laden aliyeuawa kwenye operesheni ya kijeshi nchini Pakistan.

https://p.dw.com/p/11CvZ
Waziri mkuu wa pakistan Yusuf Raza GilaniPicha: picture-alliance/dpa

Marekani imeitaka Pakistan kusaidia kuondoa hali ya kutoaminiana kwa kuwaruhusu wachunguzi wake kupata fursa ya kuwafikia wajane watatu wa Osama bin Laden, ambao wanashikiliwa nchini Pakistan na ambao ni muhimu katika kupata taarifa juu ya mtandao wa al Qaeda.

Hali ya wasiwasi imeongezeka kati ya washirika hao wawili walio katika mapambano ya kukabiliana na ugaidi katika wakati huo ambao makomando wa Marekani wamefanya shambulio lililomuua Osama bin Laden, mtu ambaye alikuwa akitafutwa zaidi duniani, shambulio ambalo lilifanywa katika eneo alilokuwa akiishi karibi na mji mkuu wa Pakistan Islamabad.

Marekani imetaka kufanya uchunguzi juu ya jinsi gani kiongozi huyo wa al Qaeda aliweza kuishi kwa miaka kadhaa katika mji wa Abbottabad uliokuwa na ulinzi na eneo ambalo liko si zaidi ya maili moja kutoka katika chuo kikubwa cha kijeshi cha Pakistan na pia mji ambao uko maili 35 tu, kutoka mji mkuu wa Islamabad.

Lakini, hata hivyo afisa mwandamizi katika serikali ya Pakistan amefahamisha leo kwamba hakuna uamuzi wowote uliochukuliwa juu ya ombi hilo la Marekani.

Pakistan imesema wake hao watatu wa Osama bin Laden, mmoja kutoka Yemen na wawili Saud Arabia pamoja na watoto zao watarejeshwa kwao na kwamba nchi hiyo imekuwa ikifanya mawasiliano na nchi zao lakini bado hazijasema kama zitawachukua.

Siku ya Jumatatu,  Waziri mkuu wa Pakistan, Yusuf Raza Gilani alizungumzia shambulio hilo na kukataa taarifa kwamba nchi yake ilikuwa imempa makaazi  mtu ambaye anaaminika kuongoza mashambulio yaliyofanywa nchini Marekani Septemba 11, mwaka 2001 na kusababisha vifo vya watu 3,000.

Osama bin Laden aliuawa kwa kupigwa risasi Mei 2 katika shambulio kubwa la siri lililofanywa katika mji wa kaskazini wa Pakistan wa Abbottabad, shambulio ambalo limeiaibisha nchi hiyo ambayo kwa miaka kadhaa imekuwa ikikanusha kwamba mtu huyo anayetafutwa duniani yuko katika ardhi yake.

Wakati huohuo, Rais Barack Obama wa Marekani amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri mkuu wa India Manmohan Singh juu ya shambulio lililofanywa na makomando wa Marekani lililomuua Osama bin Laden pamoja na kuzungumzia masuala ya usalama katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani mazungumzo hayo pia yaligusia kukua na maendeleo ya uhusiano kati ya nchi zao mbili.

Licha ya Marekani kuikosoa Pakistan kwa kushindwa kwake kumkamata Osama bin Laden, India nayo pia inailaumu nchi hiyo kwa kutochukua hatua dhidi ya wale waliopanga shambulio la Mumbai nchini India mwaka 2008 na kuua watu 166.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp, Reuters)

Mhariri: Abdul-Rahman