Marekani kuendelea na uchunguzi dhidi ya Urusi
15 Februari 2017Wademocrats wanasema uchunguzi huru ndio njia nzuri ya kujibu maswali yanayohusiana na mahusiano yaliyopo kati ya utawala wa Trump na Urusi lakini hata hivyo chama cha Republican kinaendelea kuipinga hoja hiyo na kusema kuwa uchunguzi unaoendelea hadi sasa juu ya madai hayo unatosha.
Mshauri wa usalama wa taifa Rais Donald Trump alifutwa kazi jumatatu wiki hii kutokana na kile kilichoelezwa na ikulu ya White House kuwa alimpotosha makamu wa Rais Mike Pence kuhusiana na mawasiliano yake na na balozi wa Urusi. Msemaji wa ikulu ya Marekani Sean Spicer alisema Rais Donald Trump alifahamishwa mwishoni mwa Januari kuwa Flynn alikuwana na majadiliano na balozi wa Urusi kuhusiana na suala la vikwazo dhidi ya Urusi lakini makamu wa Rais Mike Pence hakuwa na ufahamu wa taarifa hizo na hivyo kumtetea afisa huyo katika mahojiano yaliyofanywa kwa njia ya televisheni.
Hii si mara ya kwanza Rais Donald Trump kujiweka kando na mshauri wake kuhusina na suala linalohusina na Urusi. Mwishoni mwa August mwaka jana Paul Manafort alilazimika kujiuzulu kama meneja wa kampeni ya Trump baada ya shirika la habari la Asociated Press kufichua kwamba alikuwa akihusika katika kuifanyia kmpeni kwa siri chama tawala cha zamani cha Ukraine kilichokuwa kikiunga mkono Urusi.
Trump akiri urusi kufanya udukuzi wa barua pepe za Democrats
Katika utawala wa Rais Barack Obama mashirika ya kijasusi ya Marekani yalisema Urusi iliingilia uchaguzi wa mwaka 2016 ikiwa na lengo la kumuwezesha Donald Trump kushinda uchaguzi huo. Trump alikiri Urusi kufanya udukuzi wa barua pepe za chama cha Democrats lakini alikanusha hatua hiyo kuwa ilikuwa na lengo la kumuwezesha kushinda uchaguzi huo.
Gazeti la New York Times liliripoti hapo jana kuwa baadhi ya maafisa katika serikali ya Rais Donald Trump ikiwa ni pamoja na Paul Manafort walikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na maafisa wa kijasusi wa urusi kabla ya kufanyika uchaguzi wa mwaka jana ambayo Marekani ilifanikiwa kuyanasa kutokana na kufuatilia mawasiliano hayo yaliyofanywa kwa njia ya simu.
Hata hivyo Manafort alilieleza shirika la habari la Associated Press kuwa alikuwa bado hajahojiwa na Idara ya upelelezi - FBI juu ya madai hayo na kusisitiza kuwa hajawahi kufanya mazungumzo na maafisa wa kijasusi wa Urusi wala kujihusisha kwa njia yoyote ile na utawala wa Rais Putin au suala lolote linalofanyiwa uchunguzi hivi sasa.
Maafisa waliozungumza na gazeti la Times kwa sharti la kutotajwa majina wanasema hawajabaini ushahidi wowote unaohusiana na madai ya timu ya kampeni ya Trump kushirikiana na Urusi katika kufanya udukuzi au kujihusisha kwa namna yoyote katika kushawishi matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana.
Uchunguzi unaoendelea na hatua ya kufutwa kazi kwa mshauri wa masuala ya usalama w ikiwa ni siku 24 tangu aanze rasmi majukumu yake yamekiweka chama cha Republican katika hali tete yanayolazimu kuchunguzwa kiongozi wa chama hicho.
Mwandishi: Isaac Gamba/ APE/ EAP
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman