Mapungufu yajitokeza Sudan | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mapungufu yajitokeza Sudan

Nchini Sudan,matokeo ya muda ya kura ya maoni itakayoamua hatma ya eneo la kusini lililo na azma ya kujitenga yanaashiria kuwa zaidi ya asilimia 100 ya wote waliosajiliwa walifanikiwa kushiriki katika zoezi hilo.

default

Mhudumu wa Tume ya kusimamia kura ya maoni akiwa Omdurman,Sudan

Ijapokuwa kuna upungufu wa hapa na pale,hali hiyo haitarajiwi kuyabadili matokeo kamili yanayoashiria kuwa huenda eneo la Kusini likafanikiwa kujitenga.Zoezi hilo la kupiga kura ya maoni lilikamilika tarehe 15 mwezi huu na ni sehemu ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005.

Kulingana na hati hizo zilizokuwa na maelezo ya matokeo ya muda ya kura hiyo ya maoni,eneo la kusini mwa Sudan huenda likaitimiza azma yake ya kutaka kujitenga na kuwa huru.Hata hivyo upungufu ulioripotiwa kutokea huenda ukazua mitazamo tofauti na kulazimu kufuata mkondo wa sheria ili kuitatua mivutano ambayo huenda ikatokea.Maelezo hayo yametolewa na shirika la habari la Reuters.Itakumbukwa kuwa makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005 yalivimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miongo miwili.Kulingana na waangalizi wa kimataifa,zoezi hilo lilifanyika katika mazingira ya kuaminika na matokeo ya muda yaliyochapishwa kwenye mtandao wa tume iliyosimamia kura hiyo yanaashiria kuwa asilimia 99 ya wapiga kura wanaiunga mkono hatua ya eneo la Kusini ya kujitenga.Mwenyekiti wa jopo la Umoja wa Mataifa la kura ya maoni ya Sudan,rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin William Mkapa anathibitisha kuwa," Idadi hiyo ilifikiwa na zoezi hilo lilifanyika katika mazingira ya kuaminika."

NO FLASH Dschuba al-Baschir

Rais wa Sudan Omar Hassan al Bashir akiwa Juba:ameahidi kuyakubali matokeo ya kura ya maoni

Wasajiliwa wawapiku wapiga kura

Hata hivyo katika baadhi ya maeneo idadi ya waliojitokeza kupiga kura iliipiku ile ya waliosajiliwa.Hali hiyo ilidhihirika katika majimbo saba ya eneo la kusini la Equatoria,Jonglei,Upper Nile na la Magharibi.Taarifa hizo zimetolewa na shirika la habari la Reuters lilizozipata hati za tume maalum ya maandalizi wa kura ya maoni.Kwa upande wake naibu mwenyekiti wa Tume hiyo Chan Reek Madut hakulipa uzito suala hilo na alisisitiza kuwa hilo halitoyaathiri matokeo kamili yatakapotangazwa.Maelezo ya mtandao wa Tume hiyo iliyosimamia kura ya maoni yalionyesha kuwa kiasi ya wapiga kura 67,901 walisajiliwa ila ni 68,621 waliopiga kura katika eneo la Bor a wengine 84,307 walipiga kura ilhali 83,841 walisajiliwa katika eneo la Pibor jimboni Jonglei.

Waliondoka mapema

Kulingana na naibu mwenyekiti wa Tume hiyo iliyosimamia kura ya maoni,Chan Reek Madut,baadhi ya waliosajiliwa hawakuwako wakati shughuli hiyo ilipokamilika zilipochukuliwa takwimu za mwisho.

Ifahamike kuwa matokeo ya muda yanaonyesha kuwa asilimia 98.91 ya wapiga kura wanataka eneo la Sudan ya Kusini lijitenge kama yanavyoashiria matokeo kwenye mtandao rasmi wa Tume maalum iliyosimamia kura hiyo ya maoni.Kwa upande mwengine suala la Abyei bado halijatafutiwa suluhu ila huu ndio mwelekeo uliopo kulihusu kama anavyofafanua mwenyekiti wa jopo la Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan ya Kusini,Benjamin Mkapa kuwa,"Mazungumzo kati ya serikali kuu ya Sudan na ile ya Kusini hayajakamilika na yataendelea pindiu matokeo rasmi yatakapotangazwa,"alisisitiza.

Jimmy Carter Kofi Annan Sudan

Jopo la waangalizi wa kimataifa

Matokeo ya muda huenda yakatangazwa wiki ijayo baada ya kuufuata utaratibu uliowekwa :Itakumbukwa kuwa Rais wa Sudan Omar Hassan al Bashir alisema kuwa atayaheshimu matokeo ya kura hiyo ya maoni.

Mwandishi:Mwadzaya,thelma-RTRE/AFPE

Mpitiaji:Hamidou Oummilkheir

 • Tarehe 25.01.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/102RX
 • Tarehe 25.01.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/102RX

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com