Mapigano yashika kasi Syria
25 Julai 2012Helikopta za kijeshi zilishambulia leo wilaya ya al-Hajar al-Aswad mjini Damascus.
Kundi linaloangalia haki za binadamu nchini Syria limesema kuwa majeshi ya utawala wa rais Bashar al-Assad pia yametumia makombora katika mashambulio yake dhidi ya wilaya iliyoko upande wa kusini mwa mji huo mkuu.
Mji wa Aleppo katika mapigano
Majeshi ya Syria yamepelekwa kwa wingi katika mji wa Aleppo leo, ambako mashambulizi ya helikopta yamekuwa yakifanyika kuyashambulia maeneo ya waasi, na kuongeza kasi ya mashambulizi dhidi ya mji huo mkubwa kabisa nchini humo, ili kukandamiza uasi dhidi ya rais Bashar al-Assad.
Uasi nchini Syria ambao umechukua sasa miezi 16, umebadilika kutoka upinzani mdogo katika majimbo ya ndani ya nchi hiyo na kuwa mapambano makali ya udhibiti wa miji miwili muhimu, ya Aleppo na mji mkuu Damascus, ambako mapigano yalizuka wiki iliyopita.
Majeshi ya Syria yameshambulia kwa mizinga eneo la al-Tel mapema leo katika juhudi za kukamata maeneo yanayodhibitiwa na waasi, na kusababisha mtafaruku na kuwalazimisha mamia ya familia kukimbia kutoka eneo hilo, wakaazi na wanaharakati wa upinzani wamesema.
Mmoja wa watu walioshuhudia amesema:
"Hali baada ya mashambulizi hayo , ambapo maafisa wameuwawa ilikuwa hakuna chochote, hakuna mikate, hakuna maji ama umeme, hata katikati ya mji mkuu wa Damascus".
Vivuko vyadhibitiwa na waasi
Wapiganaji wa waasi ambao hawana uongozi wa kati, wamekamata karibu vituo viwili vya vivuko kuingia nchini Uturuki. Magari kadha kutoka Uturuki yameshambuliwa na kuporwa na watu wenye silaha wiki iliyopita katika kivuko cha Bab al-Hawa. Uturuki inatarajia kufunga mpaka wake na Syria baada ya wapiganaji kukamata maeneo kadha ya mpakani.
Wakati huo huo, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, amesema kuwa kuna harakati nje ya baraza la usalama la umoja wa mataifa kuunga mkono upinzani.
Washirika kutoa tamko la kuwaunga mkono waasi
"Tunafanya kazi nje ya baraza la usalama la umoja wa mataifa kutuma ujumbe wa wazi wa kuunga mkono upinzani. Kama nilivosema hapo kabla, tunatoa msaada ambao si wa mapigano. Tuna kila sababu ya kuamini kuwa hii itakuwa muhimu kwa upande wa mawasiliano, kimsingi, lakini pia msaada wa matibabu.
Silaha za sumu ziko salama
Urusi, wakati huo huo, imesema kuwa imepokea uhakikisho kutoka serikali ya Syria kuwa hazina ya silaha za kemikali iko katika usalama wa hali ya juu. Hayo yamesemwa na naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Gennady Gatilov, wakati akizungumza na shirika la habari la nchi hiyo, Itar-Tass.
Pia Urusi imeshutumu leo duru nyingine ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria.
Nae balozi wa Syria nchini Cyprus, Lamia al-Hariri, ameacha madaraka yake na kukimbilia nchini Qatar.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre/ape/dpae
Mhariri : Othman Miraji