1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yanatishia juhudi za amani Syria

15 Aprili 2016

Mapigano yameongezeka kuzunguka mji wa pili nchini Syria wa Aleppo jana Alhamis(14.04.2016), wakati mashambulizi yanayosaidiwa na ndege za kivita za Urusi yakiathiri makubaliano muhimu ya kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/1IWHo
Genf Friedensgespräche zu Syrien - Staffan de Mistura
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de MisturaPicha: Reuters/D. Balibouse

Hali hiyo hata hivyo inatishia pia duru mpya ya mazungumzo ya amani mjini Geneva.

Wapiganaji wa upande wa serikali, waasi na wapiganaji wa jihadi waliendelea na mapambano katika azma ya kupata udhibiti wa maeneo ya jimbo la Aleppo, hali inayotishia makubaliano ya karibu wiki saba sasa ya kusitisha mapigano ambayo yameshuhudia ghasia zikipungua kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka mitano ya mzozo huo.

Genf Friedensgespräche zu Syrien Vertreter der syrischen Opposition
Wawakilishi wa upande wa upinzani katika mazungumzo ya amani ya Syria mjini GenevaPicha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wakisaidiwa na ndege za kivita za Urusi wameendelea na mashambulio makali kaskazini kidogo mwa mji mkuu wa jimbo hilo Aleppo, limesema shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria.

Hatari ya kuporomosha usitishaji mapigano

Mapigano yalikuwa makubwa zaidi katika eneo la handarat, eneo la milima ambalo liko katika barabara kuu inayoelekea upande wa kaskazini katika maeneo yanayodhibitiwa na upinzani katika mji huo.

Mkuu wa shirika hilo linaloangalia haki za binadamu nchini Syria Rami Abdel Rahman amesema majeshi ya serikali, yakiungwa mkono na Urusi na ndege za kivita za Syria, yanataka kuzuwia barabara hiyo na kuzingira kabisa maeneo ya vitongoji vya upande wa mashariki.

Griechenland Flüchtlinge in Idomeni
Wakimbizi wa Syria wakiwa nchini UturukiPicha: Getty Images/AFP/D. Mihailescu

Mwandishi habari wa shirika la habari la AFP katika maeneo yanayoshikiliwa na upinzani ya mashariki mwa mji wa Aleppo amesema sauti za makombora zilisikika siku nzima jana, lakini hakuna kombora lililoangukia katika mji wenyewe hasa.

Mashambulizi hayo yamezusha , kile kilichoelezwa kuwa "wasi wasi mkubwa" katika serikali ya Marekani kuhusiana na usitishaji mapigano, ambao umeshuhudia kupungua kwa ghasia baada ya kuanza kufanyakazi Februari 27.

Marekani yaingiwa na wasi wasi

Afisa mwandamizi wa serikali ya Marekani amesema mashambulizi hayo, yanaweza kabisa kuathiri hatua ya kuacha uhasama, hali ambayo imo katika mbinyo mkubwa katika wiki za hivi karibuni.

Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini pia ameelezea wasi wasi wake juu ya mashambulizi ya Aleppo na kutoa wito wa kuheshimiwa , kuimarishwa na kupanuliwa kwa makubaliano hayo.

Rais Vladimir Putin wa Urusi muungaji mkono mkubwa wa rais Assad, amesema katika kipindi ambacho hujibu maswali ya wananchi katika televisheni ya Urusi jana kwamba anafuatilia kwa karibu ongezeko la ghasia hivi karibuni.

Federica Mogherini
Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica MogheriniPicha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

Wawakilishi wa utawala wa rais Bashar al-Assad wanatarajiwa mjini Geneva leo Ijumaa kwa ajili ya mazungumzo ya amani na mjumbe wa Umoja wa mataifa nchini Syria Staffan de Mistura, ambaye ameishutumu serikali ya Syria kwa kuzuwia juhudi za kufikisha msaada wa kukoa maisha kwa Wasyria wanaouhitaji.

"Siwezi kukana kwamba kila mmoja amekatishwa tamaa , na wengi kwa kweli wamefadhaika kutokana na kutokuwapo na misafara mipya inayofika , hususan katika maeneo ambayo yametambuliwa kuwa yamezingirwa, na pia yanatambuliwa na nyaraka za kimataifa."

Vikwazo dhidi ya IS

Urusi kwa upande wake imetoa wito jana wa kufungwa kwa mpaka kati ya Syria na Uturuki ili kuzuwia makundi ya itikadi kali ya Dola la Kiislamu na Al Nusra Front kuingiza wapiganaji na silaha kutoka nje.

UN - Ban Ki-moon im Irak
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moonPicha: Getty Images

Balozi wa Urusi katika Umoja wa mataifa Vitaly Churkin ameuambia mkutano wa baraza la Usalama la Umoja huo kuhusu kupambana na ugaidi, kwamba wajumbe ni lazima pia wafikirie juu ya kuweka vikwazo kamili vya biashara na kiuchumi dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon ameliambia baraza hilo kwamba zaidi ya watu 30,000 kutoka duniani kote wamejiunga na kampeni ya IS nchini Iraq na Syria.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape

Mhariri: Josephat Charo