1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaibuka tena Abidjan

25 Februari 2011

Mzozo unazidi kutokota nchini Cote d'Ivoire huku makabiliano mapya yakizuka baina ya majeshi yanayomuunga mkono Laurent Gbagbo na wafuasi wa mpinzani wake Alassane Ouattara Magharibi mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/10PSG
Wakaazi wa Abobo wakikimbia mapigano mjini Abidjan.Picha: AP

Hayo yanajiri huku wakaazi wa Abobo wakizidi kuuhofia usalama wao.

Wakaazi hao waliojawa hofu wametoroka eneo la Abobo lililo karibu na mji wa Abidjan huku milio ya risasi ikizidi kutanda hewani hii leo kufuatia makabiliano yaliyozuka upya magharibi mwa Cote d'Ivoire.

Hali hiyo inayotokana na kung'ang'aniwa kwa madaraka na viongozi hao wawili baada ya uchaguzi wa urais, sasa inatishia kuchochea upya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Kusambaa kwa vurumai katika taifa hilo lililo mkuzaji mkubwa wa kakao kunajiri huku juhudi za kidiplomasia za kujaribu kuutanzua mgogogoro huo baina ya Laurent Gbagbo na Alassane Ouattara, zikizidi kufifia kila kukicha.

Ouattara ndiye anayetambulika kimataifa kama mshindi wa uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba mwaka jana.

Zaidi ya watu 300 wameuwawa tangu wakati huo na hali ya usalama inayozidi kudorora wiki hii na hata kutishia uuzaji wa zao la kakao katika soko la kimataifa.

Baada ya kusikia ripoti za kuwepo kwa vikosi zaidi vinavyomuunga mkono Gbagbo, mamia ya wakaazi wakiwa na mikoba vichwani, waliondoka katika vitongoji vya Abobo, eneo ambalo kwa siku mbili zilizopita limekuwa uwanja wa mapigano baina ya majeshi ya Gbagbo na Ouattara.

Walisema kuwa walisikia tu milio ya risasi, na hawangeweza kulala hata baada ya milio hiyo kusita. Walikuwa na uoga mwingi na wakalazimika kusubiri hadi jua lichomoze ndipo waondoke makwao kukimbilia usalama wao.

Watu wa kila umri walijazana kwenye magari na kulihama eneo hilo lililo na ngome ya Ouattara, ambako nyumba zimeharibiwa na silaha nzito.

Ouattara anaishi kwenye hoteli moja katika sehemu nyingine ya mji mkuu Abidjan inayolindwa na majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa, lakini waasi wanaomuunga mkono wanaonekana kuimarisha doria zao mjini humo na kuzidisha mapambano yao katika kituo hicho cha kibiashara.

Gbagbo amekataa miito ya kumtaka ajiuzulu, licha ya matokeo ya uchaguzi yaliyokubaliwa na Umoja wa Mataifa kuonyesha kuwa Ouattara alishida katika uchaguzi huo wa terehe 28 mwezi Novemba mwaka jana, na ambao ulilenga kuliunganisha taifa hilo lakini badala yake limefungua upya migawanyiko mikali kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka wa 2002 hadi 2003.

Uchumi umeporomoka huku vikwazo vikizidi kuwekwa na zaidi ya watu laki nane wakitoroka makwao, nusu yao wakivuka hadi taifa jirani la Liberia, haya ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa ujumbe wa kulinda amani wa umoja wa mataifa nchini Cote d'Ivoire, Hammadoun Toure, amesema umoja wa mataifa unadhani kuwa makabiliano hayo yanazua hatari kubwa ya kuzuka kwa mzozo mkubwa wa matumizi ya silaha, na ambao huenda ukawa na athari zaidi kwa wananchi wa Cote d'Ivoire.

Marais wa Afrika waliotwikwa jukumu la kuutatua mgogoro huo walikuwa nchini humo wiki hii na wanatarajiwa kukutana tena hivi karibuni nchini Mauritania ili kuujadili mzozo huo lakini hakuna matumaini makubwa kuwa wataweza kupata suluhu.

Na wakati viongozi hao walipokuwa mjini Abidjan, makabiliano na umwagikaji wa damu viliendelea.

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Nigeria Odein Ajumogobia amesema kujiingiza kokote kijeshi nchini Cote d`Ivoire kutahitaji kuongozwa na Umoja wa mataifa na huenda pakatumika mkakati wa kuizingira  anga na bahari, kuliko kutumiwa wanajeshi mijini.

Mwandishi: Bruce Amani

Mhariri: Josephat Charo