1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaibuka nchini Syria huku maelfu ya waandamanaji wakijitokeza barabarani

30 Desemba 2011

Maelfu ya watu nchini Syria wamemiminika katika barabara za nchi hiyo katika maandamano makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa miezi kadhaa, wakiitisha kuvunjwa kwa utawala wa sasa wa rais Bashar al Assad.

https://p.dw.com/p/13c00
Makabiliano kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji nchini Syria
Makabiliano kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji nchini SyriaPicha: dapd

Maandamano hayo yalifanywa huku vikosi vya usalama vikiwauwa kwa kuwapiga risasi waandamanaji watano na kufyatua mabomu ya misumari katika umati wa watu kwingineko nchini humo.

Kulingana na shirika la kutetea haki za binadam la Syrian Observatory for Human Rights, maandamano ya kuipinga serikali katika mkoa unaoshuhudia ghasia wa kaskazini magharibi Idlib yalijiri baada ya sala ya waislam ya kila Ijumaa. Shirika hilo lilisema maandamano makubwa yalikuwa katika mji wa Idlib, Banash, Ariha, Sarakeb, Maaret al Numan na Khan Sheikhun miongoni mwa miji mingine.

Katika kiungani mwa mji mkuu Damascus, Douma, wanajeshi waliwafyatulia maelfu ya waandamanaji mabomu ya misumari, huku nao waandamanaji wakijibu kwa kuwarushia mawe. Utumiaji wa mabomu ya misumarí hata hivyo hakujathibitishwa kikamilifu. Mwanaharakati mmoja mjini humo aliliambia shirika hilo la Observatory kuwa alijeruhiwa na marisau kutoka kwa mabomu hayo.

Kulingana na shirika hilo, takriban waandamanaji 70,000 Wasyria walifurika kwenye barabara za Douma na walikuwa wakielekea katika ukumbi wa mji huo wakati makabiliano hayo yalipoanza. Hayo ndiyo yaliyokuwa maandamano makubwa zaidi kuwahi kufanywa katika kitongoji hicho cha kaskazini mwa mji wa Damascus tangu mwezi Machi.

Wakati huo huo zaidi ya watu 15,000 walikusanyika nje ya msikiti mkuu wa Douma ambako watu 30,000 waliandamana hapo jana. Mjini Damascus hii leo vikosi vya usalama viliwafyatulia watu risasi za moto walipokuwa wakitoka kwenye msikiti wa Akhrass katika eneo jirani la Al Kaddam. Maandamano makubwa pia yaliandaliwa katika mji wa kati wa Homs katika eneo jirani la Al Khalidiye ambako maelfu ya waandamanaji walikusanyika mahala pamoja kwa siku ya tatu mfululizo.

Umati wa watu wanaoandamana kuupinga utawala nchini Syria
Umati wa watu wanaoandamana kuupinga utawala nchini SyriaPicha: Reuters

Wanajeshi wa utawala waliwauwa takriban watu watano katika maandamano ya mjini Daraa ambako watu 17 wamekamatwa katika maeneo tofauti ya mji huo wa kusini mwa nchi hiyo.

Nalo kundi la waangalizi wa umoja wa nchi za kiarabu liliwasili leo katika mji wa Harasta karibu na Damascus na kuzungumza na wenyeji. Viongozi wa upinzani wanasema mashambulizi hayo yanayofanywa na wanajeshi wa serikali dhidi ya waandamanaji wanaotaka demokrasia yameongezeka tangu kuwasili kwa waangalizi hao mapema wiki hiikuangalia ikiwa serikali ya Syria inautekeleza mpango uliowekwa na jumuiya ya nchi za kiarabu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Othman Miraji