1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mapigano yaendelea Syria

Yamezuka mapigano baina ya majeshi ya serikali na waasi katika mji mkuu wa Syria, Damascus. Wanaharakati wanaripoti kwamba mapigano yalitokea pia katika eneo lililo karibu na Ikulu ya rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo.

Mapigano katika mji wa Damascus

Mapigano katika mji wa Damascus

Picha za video zilizotolewa katika tovuti za wapinzani wa utawala wa Assad zinaonyesha mapigano yanayosemekana kutokea huko Kfar Soussa, eneo lililo karibu na ikulu ya rais. Wanaharakati wanaeleza kwamba mapigano yalianza jana jioni na kuendelea hadi leo asubuhi. Mapigano haya ni makali zaidi kutokea mjini Damascus tangu kuanza kwa vita dhidi ya utawala wa rais Assad miezi 16 iliyopita.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu Syria na lenye makao yake makuu London, Uingereza, Rami Abdel Rahman, ameeleza kwamba mapigano makali zaidi katika mji wa Damascus yalitokea kwenye mitaa ya Tadamon, Kfar Sousa, Nahr Aisha na Sidi Qadad. Mkurugenzi huyo amefafanua kwamba vikosi vya Syria vinajaribu kuiweka mitaa hiyo chini ya utawala wake lakini hadi sasa vimeshindwa kufanya hivyo.

Kofi Annan atafanya mazungumzo na Urusi

Kofi Annan atafanya mazungumzo na Urusi

Mapigano haya yanakuja muda mchache kabla ya mjumbe maalum wa kuleta amani Syria, Kofi Annan, kufanya ziara nchini Urusi na kuiomba nchi hiyo imwekee Assad shinikizo zaidi ili asimamishe machafuko. Urusi na China, nchi ambazo ni washirika wa karibu wa Syria, zinapingana na nchi za Magharibi na za Kiarabu zinazotaka kupitisha azimio la Umoja wa Mataifa ambalo litatishia kumwekea Assad vikwazo iwapo atashindwa kusimamisha vita nchini mwake na kuleta mabadiliko ya kisiasa.

Wapinzani walilengwa Tremseh

Askari mmoja wa Syria aliyelikimbia jeshi, Meja Jenerali Adnan Salo, ameliambia gazeti la Asharq al-Awsat kwamba waasi hivi sasa wanadhibiti asilimia 60 ya eneo la Syria na hivyo kinachohitajika ni majeshi ya NATO kuingia nchini humo ili kusaidia kumng'oa rais Assad madarakani. "Kinachohitajika sasa ni mashambulio mawili ya angani katika ikulu ya rais, baada ya hapo tutaweza kutawala miji yote ya Syria," alisema jenerali huyo aliyekuwa mkuu wa kikosi cha silaha za kemikali.

Nyumba iliyoharibiwa katika shambulizi la Tremseh

Nyumba iliyoharibiwa katika shambulizi la Tremseh

Wakati huo huo, ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria umeeleza kwamba mauaji ya watu wasiopungua 200 yaliyofanyika wiki iliyopita katika kijiji cha Tremseh yalikuwa na lengo maalum. Msemaji wa ujumbe huo, Sausan Gosheh, ameeleza kuwa waliolengwa hasa walikuwa wanaharakati na wapinzani wa Assad. "Tunaweza kuthibitisha kwamba Alhamisi iliyopita palifanyika operesheni ya kijeshi. Mashambulizi yalilenga nyumba za wanaharakati na za maaskari waliolikimbia jeshi," alisema Gosheh. "Tumekagua baadhi ya nyumba na kukuta madimbwi ya damu pamoja na magamba ya risasi. Silaha nyingi sana zimetumika, zikiwemo silaha nzito kama mizinga, maguruneti na risasi. "

Hata hivyo msemaji wa serikali ya Syria amekanusha madai hayo na kusema kwamba jeshi la nchi yake halikutumia silaha nzito na kwamba waasi ndio walioanza kukishambulia kijiji cha Tremseh.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com