1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaendelea mjini Tripoli

25 Agosti 2011

Mapambano yanaendelea nchini Libya, vikosi vya Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi vinapigania kuyaresha katika himaya yao makaazi ya kiongozi wao, ikiwa ni siku moja baada ya kudhibitiwa na waasi

https://p.dw.com/p/12NRc
Waasi wakipambana katika eneo la Bab al-AziziyaPicha: dapd

Mapambano yanaendelea nchini Libya, vikosi vya Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi vinapigania kuyaresha katika himaya yao makaazi ya kiongozi wao, ikiwa ni siku moja baada ya kudhibitiwa na waasi, wakati huohuo waasi hao wametangaza kitita cha euro milioni 1.7 kwa yeyote atakaefanikisha kupatikana kwa kiongozi huyo akiwa hai au amekufa.

Wakati hayo yakiendelea Marekani na Qatar kwa shabaha ya kuwaunga mkono waasi zipo katika jitihada za kidiplomasia za kufanikisha kutolewa kwa fedha za Libya zilizozuiliwa ili zisadie waasi hao.

Marekani kwa upande wake imesema tatizo la silaha za maangamizi nchini Libya limekwisha na kwamba ina uhakika kwamba Baraza la Mpito la Waasi litaweza kuandaa muundo wa serikali baada ya kudhiti Tripoli.

Flash-Galerie Libyen Journalisten im Rixos-Hotel
Waandishi waliozuiwa Hotelini mjini TripoliPicha: picture alliance/dpa

Kundi la waandishi wa habari wa kigeni waliozuliwa na vikosi vya Gaddafi katika hoteli ya Rexos mjini humo wameachiwa huru, lakini kundi lingine la vikosi hivyo limewateka waandishi wa habari wannne kutoka Italia pembezoni mwa mji huo.

Aidha wale waandishi wengine wa habari waliojeruhiwa katika mapigano yanayoendelea katika makazi ya Gaddafi wanaendelea vizuri.

Waasi pia wameweza kufanikisha uhusiano muhimu wa kidiplomasia na Chad pamoja na Burkina Faso. nchi hizo zimelitambua baraza hilo kama chombo halali chenye kuwakilisha wananchi wa Libya.

Moshi mkubwa ulitanda katika eneo la Bab al-Aziziya eneo ambalo waasi na majeshi ya Gaddafi yamekuwa yakishambuliana kwa kutumia silaha mbalimbali zikiwemo mizinga na maroketi.

Msemaji wa waasi aliiambia televishini ya Al-Jazeera kwamba mpaka sasa wanadhibiti kati ya asilimia 90 hadi 95 za mji wa Tripoli huku akiongezea kusema kwamba kudhibiti makazi ya Gaddafi ya Bab al-Aziziya ni ishara kwamba utawala wake wa miaka 41 umemalizika.

Hata hivyo televisheni ya Al-Jazeera hivi punde ilifanya mahojiano ya moja kwa moja kwa njia ya simu na mkazi mmmoja wa Tripoli Mariam Wafa ambae alisema hali ya usalama katika mji huo sio nzuri hata kidogo.

" Nataka kutuma ujumbe maaalumu kwa wakazi wote wa Tripoli, tafadhali, bakini majumbani kwa kuwa mji sio salama, kumejaa watunguaji, hata kama mji upo katika udhibiti wa waasi, mji sio salama, ukweli kunahitajika uangalifu" alisema Mariam.

Televishini hiyo pia imeaonyesha idadi kubwa ya wagonjwa katika baadhi ya mahospitali ambapo hivi sasa inadaiwa kuwepo kwa zaidi ya majeruhi 2,000 huku vikiripotiwa vifo 400 tangu waasi kuingia katika mji huo.

Kwingineko, huko Uingereza, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Liam Fox aliiambia Sky news kwamba Umoja wa Kujihami wa NATO, unatoa misaada ya kipelelezi na kijaasusi kwa waasi katika jitihada za kumsaka Gaddafi.

Hata hivyo waziri huyo amekanusha taarifa za zilizoandikwa na gazeti moja nchini humo kwamba Uingereza imetuma kikosi maalum cha kijeshi cha ardhini katika mji wa Tripoli.

Mwandishi: Sudi Mnette/ RTR
Mhariri:Yusuf Saumu