1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano nchini Tchad

Oumilkher Hamidou8 Mei 2009

Vikosi vya serikali vinaendelea kupigana na waasi karibu na Abeche

https://p.dw.com/p/Hlzm
Wakimbizi wa Sudan nchini TchadPicha: AP

Mapigano makali yanaendelea kati ya vikosi vya waasi na vile vya serikali ya Tchad karibu na Abéché, mashariki ya nchi hiyo, si mbali na mahala ambako kambi hizo mbili zilipigana pia hapo jana.

"Mapigano haya yaliyoripuka tangu alfajiri,yanaendelea Houaich, karibu na Am-Dam, umbali wa kilomita 100 kusini mwa Abéché. Mapigano hayo yametuwama karibu na mahala wanakoishi wakimbizi karibu laki nne na nusu wa Sudan na Jamhuri ya Afrika kati.

Serikali inasema imewauwa waasi 125 na kupotelewa na wanajeshi wake 21.Waasi wengine 152 wamekamatwa.

Muungano wa vikosi vya upinzani-UFR, unaoyaleta pamoja makundi tisaa ya waasi, haujatangaza hasara ya maisha iliyopatikana.

Rebellen in tschadische Hauptstadt N'Djamena eingerückt
Waasi wa UFR nchini TchadPicha: picture-alliance/dpa


Katika taarifa yake iliyochapishwa mjini Libreville,nchini Gabon- naibu msemaji wa wa UFR amezungumzia juu ya "dazeni kadhaa za waliokufa na kujeruhiwa" na wanajeshi kadhaa wa serikali waliokamatwa sawa na vifaru kadhaa vilivyoharibiwa na magari mengine ya kijeshi kuripuliwa."

Msemaji wa UFR,Abderaman Koulamallah anasema wamewashinda nguvu wanajeshi wa serikali na wanaudhibiti kikamilifu mji wa Am-Dam.

Waasi hao wa UFR wamejipenyeza tangu May nne iliyopita wakitokea Sudan,na wanadai lengo lao ni "kuutimua madarakani utawala wa rais Idriss Derby mjini Ndjamena".

Marekani imelaani vikali mashambulio hayo ya waasi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje Robert Wood amesema katika taarifa tunanukuu: "Marekani inaunga mkono usalama,utulivu na umoja wa Tchad".Mwisho wa kumnukuu msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya marekani aliyewatolea mwito waasi wasitishe opereshini zao zote,waachane na matumizi ya nguvu na waanzishe mazungumzo pamoja na serikali ya Tchad ili kujiunga na maisha ya kijamii nchini Tchad.

Marekani imeitolea mwito pia serikali ya mjini Ndjamena iwapokonye silaha waasi wote na ihakikishe wanarejea nyumbani haraka.

Sudan na Tchad,zinazolaumiana kuwaunga mkono waasi wa kila upande,zimetiliana saini jumapili iliyopita,mjini Doha,Qatar , makubaliano ya kusaka suluhu baina yao. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imezitolea mwito nchi hizo zote mbili ziheshimu makubaliano hayo.

Na baraza la Usalama la umoja wa mataifa linatazamiwa kukutana leo hii kuzungumzia hali namna ilivyo nchini Tchad.

Mwandishi: Oummilkheir Hamidou

Mhariri: Miraji Othman