1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yaongezeka Jerusalem

Sekione Kitojo
23 Julai 2017

Israel imetuma wanajeshi zaidi katika eneo la Ukingo wa Magharibi siku ya Jumamosi(22.07.2017)na vikosi vya polisi vilivunja mkusanyiko wa Wapalestina waliokuwa wakirusha mawe mjini Jerusalem na  wasi wasi ukiongezeka. 

https://p.dw.com/p/2h1FU
Israel - Palästina - Konflikt - Unruhen
Picha: picture alliance/abaca/I. Rimawie

Wizara ya afya  ya  Palestina imesema Mpalestina  mmoja ameuwawa  katika  mapambano  tofauti  nje  ya  mji  huo, na kufikisha  idadi ya  watu  waliouwawa  katika  muda  wa  siku  mbili zilizopita  kuwa  saba. Hata  hivyo wizara  hiyo  haikutoa  maelezo zaidi ya  vipi mtu huyo alifariki.

Waisraeli wawili  walichomwa  visu  na  kufariki siku  ya  Ijumaa wakati  wakila  chakula  cha  jioni  katika  makaazi  ya  Wayahudi katika  Ukingo  wa  Magharibi.

Jerusalem Tempelberg Unruhen Polizei Protest
Waandamanaji wakitawanywa na polisi mjini JerusalemPicha: Reuters/R.Zvulun

Masaa  kadhaa  mapema, Wapalestina  wawili  waliuwawa  katika ghasia  zilizozushwa  kutokana  na  Israel  kuweka  vifaa  vya ukaguzi  katika  eneo  la  kuingilia  katika  eneo  hilo  takatifu katika mji mkongwe uliozungushiwa ukuta.

Urusi, Marekani , Umoja wa Ulaya  na  Umoja  wa  mataifa , kile kinachofahamika  kwa jina  la  pande  nne za upatanishi wa  amani katika  mashariki  ya  kati , wamesema  katika  taarifa  ya  pamoja kwamba "wana wasi  wasi  mkubwa  kutokana  na  hali  ya  wasi wasi  inayoongezeka na  ghasia  na mapambano  yanayotokea ndani  na  kuzunguka  mji  mkongwe  wa  Jerusalem", na  kutoa  wito wa  kujizuwia  kwa  pande zote  mbili.

Israel - Palästina - Konflikt - Unruhen
Wapalestina wakirusha mawe kwa polisi na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa MagharibiPicha: Reuters/I. A. Mustafa

Baraza la Usalama kujadili hali ya vurugu

Wanadiplomasia  wamesema baraza la Usalama  la  Umoja  wa mataifa  litakutana  kujadili hali  hiyo  Jumatatu. Sweden , Misri  na Ufaransa  zimeomba  mkutano  huo "kujadili kwa  haraka  vipi  miito ya  kupunguza  hali  ya  wasi  wasi  mjini  Jerusalem  inaweza kuungwa  mkono", mratibu wa  baraza  la  usalama  la  Sweden , Carl Skau, aliandika  katika  ukurasa  wa  Twitter.

Rais  wa  palestina Mahmoud Abbas ameamuru kusitishwa kwa mahusiano yote  rasmi na  Israel  hadi  pale Israel  itakapoondoa vifaa  hivyo  vya  ukaguzi vya  kugundua  vitu vya  cuma  katika eneo  hilo  takatifu mjini  jerusalem, mahali  ambapo Waislamu wanasali  katika  msikiti  wa  al-Aqsa. Hakutoa  maelezo  zaidi, lakini mahusiano  ya hivi  sasa  ni  kwa  kiwango  cha  chini  katika ushirikiano  wa  kiusalama.

Palästina Ramallah Mahmoud Abbas
Rais wa Palestina Mahmoud AbbasPicha: picture-alliance/abaca

Baraza la mawaziri linalohusika na usalama la Israel  linatarajiwa kuketi leo Jumapili (23.07.2017) na linatarajiwa  kujadili hatua mbadala  za  kiusalama ambazo zinaweza  kutumika  badala ya  vifaa hivyo  vya  kugundua vitu vya  chuma, kwa  mujibu wa  maafisa wawili  wa  Israel , ambao  wameomba majina  yao  kutotajwa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Sudi Mnette