Maoni ya wahariri,juu ya Syria,Ugiriki na Napolitano
23 Aprili 2013Gazeti la "Emder" linatoa juu ya uamuzi wa Ugiriki na Cyprus wa kuwapa vibali vya kuishi nchini wawekaji vitega uchumi ambao si raia wa Umoja wa Ulaya.Serikali za nchi hizo zitatoa vibali hivyo kwa wafanyabiashara watakaonunua au kukodi mali katika sekta ya ujenzi thamani ya Euro zaidi ya laki mbili na nusu.Lengo la uamuzi huo ni kuifufua sekta ya ujenzi.
Juu ya uamuzi huo gazeti la"Emder" linasema ni vizuri kwamba serikali za nchi hizo zinajaribu kuwa na ubunifu katika juhudi za kupambana na mgogoro wa madeni. Hata hivyo gazeti la "Emder"linasema uamuzi huo unatoa picha kwamba yeyote mwenye fedha anaweza kuununua uraia wa Umoja wa Ulaya.Gazeti hilo linauliza jee sera hiyo itaipeleka wapi Ulaya? Nchi nyingine za Ulaya zinapaswa kuchukua hatua za haraka ili kuizuia sera hiyo
Silaha kwa wapinzani, Syria?
Umoja wa Ulaya umelegeza vikwazo dhidi ya Syria. Kulingana na uamuzi huo nchi za Umoja huo zitaruhusiwa kuyanunua mafuta ya Syria yanayodhibitiwa na wapinzani wa serikali. Lakini Uingereza na Ufaransa zinataka vikwazo vya silaha pia viondolewe. Lakini Ujerumani inaupinga mtazamo huo.
Gazeti la "Straubinger Tagblatt" linatoa maoni juu ya msimamo huo wa Ujerumani kwa kusema kwamba msimamo huo ni sahihi hata ikiwa unaonekana kuwa siyo wa kiungwana.Sababu ni kwamba hakuna anaeweza kutoa uhakika kwamba silaha kutoka Ujerumani hazitatumika kwa ajili ya kupigania kuunda nchi ya itikadi kali ya kiislamu. Uamuzi wa kulegeza vikwazo vya mafuta ni sahihi,kwa sababu vikwazo hivyo vimewaathiri zaidi wananchi kuliko utawala wa kidhalimu wa Hafez al.Assad. Na ili kuwasaidia wananchi wa Syria, kinachotakiwa ni maendeleo ya kiuchumi badala ya kuwapa mahema na mikate ya resheni.
Napolitano achaguliwa tena:
Gazeti la "Neue Osnabrücker "linatoa maoni juu ya kuchaguliwa tena kwa Giorgio Napolitano kuwa Rais wa Italia.Mhariri wa gazeti hilo anasema kuchaguliwa tena kwa Napolitano kuwa Rais wa Italia kunathibitisha adhma na hisia za kuwajibika za kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 87.Ni jambo la hakika kwamba Italia ingelikuwa na uwezo wa kuyatatua matatizo mengi, laiti pengekuwapo watu wengi kama Napolitano.Lakini kwa bahati mbaya watu kama yeye hawapo. Na badala yake vipo vyama vya kisiasa vinavyokingamana,kuchafuliana sifa na kushikilia upinzani. Mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker" amesema kwa mambo hayo mtu anagonga vichwa vya habari, lakini hajengi nchi.
Mwandishi:Mtullya Abdu /Deutsche Zeitungen.
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman