1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

16 Agosti 2007

Katika maoni yao leo, wahariri wa magazeti takriban yote ya Ujerumani wanazungumzia juu ya kuuawa polisi watatu wa Ujerumani nchini Afghanistan.

https://p.dw.com/p/CHS7


Polisi watatu wa Ujerumani wameuawa katika shambulio la kigaidi mjini Kabul mkasa ambao kwa mara nyingine umezusha mjadala mkali hapa nchini juu ya jukumu la kulinda amani linalotekelezwa na wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan.


Baadhi ya wahariri wanasema huenda mkasa huo ukaongeza idadi ya wabunge wanaopinga jukumu la kulinda amani nchini Afghanistan linalotekelezwa na wanajeshi wa Ujerumani.

Hayo ndiyo anayosema mhariri wa gazeti la LANDESZEITUNG kutoka mji wa Lüneburg kaskazini mwa Ujerumani.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa kila tukio la kigaidi litakalosababisha vifo vya askari wa Ujerumani litaongeza idadi ya wabunge wanaopinga kuwepo askari wa Ujerumani nchini Afghanistan. Mhariri huyo anatilia maanani kwamba chama cha Social Demokratik ambacho kimo katika serikali ya mseto ya Ujerumani sasa kimebanwa kutokana na kushambuliwa na kambi ya mlengo wa kushoto inayopinga katu katu kupelekwa wanajeshi wa Ujerumani kulinda amani nchini Afghanistan.

Lakini mhariri wa gazeti hilo anawakumbusha hao wanaopinga jukumu la kulinda amani nchini Afghanistan juu ya yaliyotokea nchini Rwanda na katika eneo la Balkan hapa barani Ulaya.

Mhariri huyo anawakumbusha watu hao juu ya aliyosema aliekuwa Kansela wa Ujerumani mnamo miaka ya 80 Willy Brandt kwamba katika mazingira ya migogoro isiyoeleweka haiwezekani kulinda amani bila ya kutumia ncha ya upanga.

AM.