1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri.

2 Oktoba 2007

Rais Horst Köhler wa Ujerumani amekosoa sera za dunia utandawazi ambazo amesema zinawapunja masikini duniani. Katika maoni yao, wahariri wa magazeti ya leo wanazungumzia juu ya lawama za rais huyo.

https://p.dw.com/p/CHRi

Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya mjadala uliopo ndani ya chama cha Social Demokratik juu ya malipo yanayotolewa kwa watu wasiokuwa na ajira hapa nchini.

Mhariri wa gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG anasema rais Köhler ameeleza wazi kwamba katika sera za dunia utandawazi nchi masikini zinasibika kutokana na tabia ya undumakuwili katika biashara.

Gazeti limetilia maanani kauli ya rais huyo juu ya vizingiti vinavyowekwa na nchi tajiri katika biashara baina yao na nchi zinazoendelea. Rais wa Ujerumani pia amezikosoa nchi za viwanda kwa kujaza bidhaa zinazouzwa kwa bei ya kutupa kwenye soko la dunia.

Gazeti linasema kauli ya rais Köhler siyo jambo la kukurupuka bali ni mtazamo unaolenga shabaha inayoeleweka.Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani ,haja aliyosisitiza rais Köhler , kuzitaka nchi tajiri zijenge njia mpya katika uhusiano wao na nchi zinazoinukuia kiuchumi, na nchi nyingine zote zinazoendelea .

Mhariri wa gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG anamaliza kwa kusema kwamba kauli ya rais wa Ujerumani ni mapinduzi ya kisiasa na kiuchumi.

Juu ya kauli ya rais Köhler gazeti la DIE WELT linasema kwamba mtazamo wa rais huyo unaonesha kuwa inawezekana kuzungumza na wajerumani bila ya kuwakaripia, na kuwaomba wachukue hatua zaidi.

Lakini mhariri wa gazeti la OST THÜRINGER anauliza iwapo rais Köhler amepata kitu kipya cha kuzungumzia kwa kutoa kauli hiyo ya kukosoa sera za dunia utandawazi?

Anachosema mhariri huyo ni kwamba rais Köhler anaweza kutoa kauli kama hizo za kutoa nasaha na miito ya busara na kwamba yote hayo yanaingia vizuri katika masikio ya wananchi. Lakini gazeti linasema , kisiasa nasaha hizo ,hazimfikishi mbali.

Katika maoni yao wahariri leo pia wanazungumzia juu ya pendekezo la mwenyekiti wa chama cha Social Demokratik juu ya kurefusha muda wa kulipa posho kwa watu wasiokuwa na ajira.

Gazeti la RHEIN-NECKAR kutoka mji wa Heidelberg linamkosoa mwenyekiti huyo wa wa SPD.Gazeti hilo linaeleza kuwa mwenyekiti huyo bwana Kurt Beck anataka muda huo urefushwe kutoka mwaka mmoja na nusu hadi miaka miwili. Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema pendekezo hilo linaweza kukigawa chama chake cha SPD.

Gazeti hilo pia linasema bwana Beck anakusudia kutumia pendekezo hilo katika kampeni yake ya uchaguzi wa mwaka 2009. Lakini amechelewa, linasema gazeti hilo.

Lakini gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG linasema pana haja ya kufanyika mageuzi.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa aliefanya kazi kwa miaka mingi na kulipia bima ya wasiokuwa na ajira kwa miaka mingi, anahisi kuwa anaadhibiwa mara mbili kwa kulipwa posho ya wasiokuwa na ajira kwa muda mfupi . Sababu ni kwamba baada ya muda wa mwaka mmoja tu , ikiwa mtu huyo hatapata ajira nyingine ,basi ataporomoka kimaisha na kuwa mwombaji wa msaada wa kijamii.