1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gauck amaliza ziara ya China

Admin.WagnerD24 Machi 2016

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya mjadala unaohusu usalama barani Ulaya na pia wanazungumzia juu ya ziara ya Rais wa Ujerumani Joachim Gauck nchini China.

https://p.dw.com/p/1IIk9
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck
Rais wa Ujerumani Joachim GauckPicha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Juu ya mjadala kuhusu usalama wa bara la Ulaya mhariri wa gazeti la "Rhein-Zeitung" anasema kwanza inapasa nchi za Ulaya ziwe makini katika ukusanyaji wa data- yaani habari muhimu zitakazowezesha kufikia shabaha zinazolengwa. Hata hivyo mhariri wa gazeti hilo analitilia maanani suala la ulinzi wa data- na hasa ulinzi wa habari juu ya watu binafsi.

Mhariri huyo anauliza ni kiasi gani cha habari kinachostahili kulindwa na wakati huo huo ,kuweza kuleta usalama zaidi ? Gazeti la "Rhein -Zeitung" linasema wakati sasa umefika wa kuwapa walinzi wa usalama kile ambacho wamekuwa wanakisubiri kwa muda mrefu!

Gazeti la "Volksstimme" linaizungumzia ziara ya Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier nchini Urusi. Mhariri wa gazeti hilo anasema yapo masuala ya utata yanayopaswa kujadiliwa baina ya Ujerumani na Urusi- mgogoro wa mashariki mwa Ukraine na mgogoro wa Syria.

Lakini mhariri wa gazeti hilo pia anasisitiza kwamba namna ya kuutatua mgogoro wa mashariki mwa Ukraine na mustakabal wa Rais Bashar al-Assad ni mambo muhimu, lakini hatari inayotokana na ugaidi ni hatari kubwa zaidi.

Gazeti linasema magaidi wa Daesh- yaani "dola la Kiislamu" wanatishia usalama wa Ulaya ya kati na ya mashariki , ikiwa pamoja na wa Urusi. Tofauti na hapo awali,Urusi sasa inaamua yenyewe ni nani wa kushirikiana naye katika harakati za kupambana na magaidi katika ushirika wa usawa. Katika hilo, Ujerumani ni chaguo la kwanza kwa Urusi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: Getty Images/AFP/Y. Kadobnov


Rais wa Ujerumani Joachim Gauck anaendelea na ziara ya China alitumia maneno makali kuukosoa utawala wa kikomunisti katika iliyokuwa Ujerumani Mashariki. Lakini katika maoni yake mhariri wa gazeti la "Süddeutsche" anasema Bwana Gauck hakusema ambacho hasa alipaswa kusema.

Mhariri huyo anaeleza kwamba Gauck alipaswa kusema kwamba Ujerumani haikubaliani asilani na ukiukaji wa haki za binadamu nchini China. Lakini Rais wa Ujerumani alieupuka kutamka hayo. Na jee laiti angelisema pangelitokea nini? Kuharibika kwa uhusiano baina ya China na Ujerumani? Potelea mbali! Angeliwalenga wale wanaostahili.

Katika hotuba yake mjini Shanghai, Rais wa Ujerumani aliwasilisha ujumbe uliosema kwamba ukomunisti , hauwezi kuwa ruwaza ya maendeleo siku za usoni.Mhariri wa gazeti la "Westfälische Nachrichten" anasema Bwana Gauck ameuwasilisha ujumbe huo katika wakati na mahala mwafaka!

Mwandishi:Mtullya Abdu. Deutsche Zeitungen:

Mhariri:Yusuf Saumu