1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAONI YA WAHARIRI

Abdu Said Mtullya31 Oktoba 2011

Jee msaada wa China ni hatari kwa nchi za Ulaya?

https://p.dw.com/p/132GP
Rais Heinz Fischer, wa Austria (kulia) na Rais wa China Hu Jintao mjini Vienna. Jee China ni hatari kwa nchi za Ulaya ?Picha: dapd

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni juu ya msaada wa China kwa nchi za Ulaya na juu ya kauli iliyotolewa na Rais Bashar al- Assad wa Syria.


Gazeti la Der Tagespspiegel linaitilia maanani, hali halisi inayozikabili nchi za Ulaya katika uhusiano wao na China. Mhariri wa gazeti hilo anasema kwamba nchi za Ulaya sasa zinauhitaji msaada wa China ili kuweza kuukabili mgogoro mkubwa wa madeni.

Mhariri huyo anatilia maanani kwamba kwa baadhi ya nchi, China ni hatari! Lakini anasema kile kinachozingatiwa kuwa ni hatari kwa nchi za Ulaya kuitegemea China, imekuwa hali halisi tokea siku nyingi. Na jambo muhimu kulitambua anasema mhariri wa Der Tagesspiegel ni kwamba Ulaya na China ni pande zinazotegemeana; kwa sababu hata ikiwa Ulaya inauhitaji msaada wa China, China nayo inazihitaji nchi za Ulaya kwa kila hali. Mhariri wa Der Tagesspigel anaeleza kuwa Ulaya ni mshirika mkuu wa biashara wa China.


Mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine anayazungumzia matukio ya nchini Syria na anatoa maoni yake juu ya kauli ya Rais Bashar al-Assad. Anasema anaepiga mayoe kizani ni mtu mwenye hofu. Usemi huo unaweza kutumiwa kuhusiana na kauli iliyotolewa na Rais Bashar al- Assad. Rais huyo ameionya jumuiya ya kimataifa dhidi ya kujiingiza katika mambo ya ndani ya Syria. Huo ni msamiati wa kawaida .Lakini onyo alilolitoa kwamba Syria itageuka Afghanistan nyingine endapo mataifa fulani yatakifuafa kigezo cha Libya lapaswa kuzingatiwa kwa makini.

Gazeti la Neue Osnabrücker linazungumzia juu ya maanufaa ya kuwaleta nchini Ujerumani wafanyakazi wa kituruki miaka 50 iliyopita.

Mhariri wa gazeti hilo anasema pamoja na manufaa makubwa yaliyopatikana haitafaa kuyafumbia macho matatizo yaliyopo. Mhariri huyo anaeleza kwamba manufaa ya mkataba wa kuwaleta wafanyakazi wa Kituruki kufanyakazi nchini Ujerumani, miaka 50 iliyopita, yanaivuka mikataba iliyotiwa saini baina ya Ujerumani na Italia,Uhispania na Ugiriki.

Idadi ya wafanya kazi wahamiaji kutoka Uturuki iliivuka ile ya nchi hizo nyingine. Waturuki wamenufaika na mkataba huo hasa kutokana na kuweza kupeleka nyumbani fedha za kigeni. Lakini Ujerumani pia imenufaika na nguvu kazi ya wafanyakazi wahamiaji kutoka Uturuki. Hata hivyo,pamoja na mafanikio yaliyopatikana, haitakuwa sawa kuyafumbia macho matatizo yaliyopo .

Mwandishi/Mtullya Abdu/Duetsche Zeitungen/

Mhariri/Josephat Charo/