Maoni ya wahariri wa magazeti | Magazetini | DW | 18.09.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya mdajala kuhusu usalama wa ndani nchini Ujerumani na juu ya mpango wa kubinafsisha sehemu ya shirika la reli la Ujerumani. Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya hukumu iliyotolewa dhidi ya kampuni ya Microsoft.


Waziri wa ulinzi wa Ujerumani bwana Franz Joseph Jung amesema kuwa hatasita kutoa amri ya kuitungua ndege yoyote iliyotekwa nyara kwa madhumuni ya kufanya mashambulio ya kigaidi nchini Ujerumani.Kauli hiyo imesababisha mzozo miongoni mwa baadhi ya wanasiasa na wananchi wengine kadhalika.Juu ya hayo mhariri wa gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE anamlaumu waziri Jung kwa kutoa kauli hiyo.

Mhariri huyo anasema, kwa mara nyingine suala la usalama wa taifa linatumiwa vibaya ili kuiwezesha nchi kuchukua hatua zinaoenda kinyume cha haki na maadili.

Gazeti hilo linaongeza kwa kutilia maanani kwamba katika nyakati hizi za hatari, wajerumani wanahitaji nchi inayotambua kwamba, ugaidi unaweza kupigwa vita kwa uthabiti wote , lakini katika misingi ya sheria.

Naye mhariri wa gazeti la DARMSTÄDTER ECHO anaeleza kuwa kauli ya waziri wa ulinzi imesababisha mtafaruku miongoni mwa marubani vile vile. Gazeti hilo linatilia maanani mtanziko utakaowakabili marubani hao , jee watalazimika kutii amri ama kufuata katiba?

Na gazeti la FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND linamwambia waziri Jung kuwa yeyote anaedhamiria kuwaweka wanajeshi nje ya katiba ili atimize shabaha zake ,basi mtu huyo hana la maana la kusema.

Gazeti hilo pia linamtaka Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amkazie macho waziri wake wa ulinzi.

Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya mpango wa kubinafsisha sehemu ya shirika la reli nchini Ujerumani.

Gazeti la DER NEUE TAG linawaambia wasomaje wake kuwa yeyote anaetaka kujua yatakayotokea kwa shirika la reli baada ya kubinafishishwa anapaswa kuangalia yanayofanywa na makampuni binafsi ya nishati ya umeme nchini Ujerumani.Mhariri anasema makampuni hayo yanadhiti soko lote la nishati kiasi, kwamba hakuna tena ushindani wa haki.

Gazeti la SÄCHSICHE ZEITUNG linazungumzia hukumu iliyotolewa kwa kampuni ya kampyuta ya Microsoft. Kampuni hiyo imepigwa faini ya Euro milioni 497 kwa kukiuka taratibu za ushindani. Gazeti linasema adhabu hiyo ni ujumbe kwa makampuni mengine yote yenye tabia ya ukiritimba. Gazeti hilo linasema adhabu hiyo ni ushindi wa kanuni za biashara huru na ya haki.