Magazetini
27 Januari 2010Tume ya wabunge nchini Ufaransa imependekeza kupigwa marufuku kwa vazi linalofunika mwili mzima.
Magazeti ya Ujerumani leo yanatoa maoni yao juu ya suala hilo.
Lakini wahariri hao pia wanaungumzia juu ya uhusiano baina ya Israel na Ujerumani.
Tume ya wabunge kutoka vyama vyote vikuu nchini Ufaransa inataka watu wapigwe marufuku kuvaa, hadharani kwa vazi linalofunika mwili wote, yaani burka,
Gazeti la Volksstimme linasema watu barani Ulaya tayari inawawia vigumu kuwaona akina mama wa kiislamu wakivaa hijab tu, sembuse Burka, linalofunika mwili mzima.
Gazeti hilo linasema, vazi la Burka limevuka mipaka yote.
Mhariri wa Volkstimme anaeleza kuwa vazi hilo halitangamani na utamaduni wa kifaransa kama vile jinsi kichupi cha upati-yaani bikini kisivyoweza kukubalika katika utamaduni wa Yemen.
Kwa hiyo rais Sarkozy wa Ufaransa amesema vazi la Burka halitakiwi, na linapaswa kupigwa marufuku.
Gazeti linasema msimamo wa rais huyo hauwafiki na jamii yenye tamaduni mbalimbali-jamii ambayo kwa kawaida inahakikisha uhuru wa mavazi kwa wananchi wote. Kwa hiyo Sarkozy anapaswa kusema wazi kwamba stahamala ya demokrasia sasa imefikia mwisho nchini Ufaransa.
Lakini gazeti la Allgemeine Zeitung linaunga mkono msimamo wa rais Sarkozy kwa kusema
kwamba kila raia mwema katika nchi anapaswa kuwa na uhusiano mzuri na jirani yake bila ya kujali iwapo jirani huyo ana nasaba ya uhamiaji ama la. Lakini haina maana kwamba raia mwema huyo akubali kila kitu cha jirani yake, hata kile ,kinachoenda kinyume na utamaduni wake.
Gazeti la Braunschweiger leo linazungumzia juu ya uhusiano baina ya Ujerumani na Israel kwa kutilia maanani historia ya nchi hizo mbili.
Gazeti hilo ,linaeleza kuwa yaliyotokea katika miaka ya nyuma bado ni zigo kubwa, linalowalemea wajerumani. Na hakuna maneno yanayotosheleza kulielezea zigo hilo.
Ndiyo sababu anatamka mhariri wa gazeti hilo kuwa ni sahihi kwamba rais Horst Köhler wa Ujerumani ametoa mwito wa kuendelea kuyakumbuka yaliyotokea mnamo miaka ya nyuma baina ya wajerumani na wayahudi. Mhariri wa gazeti la Brauschweiger anasisitiza kwamba, ili kujenga mustakabal mzuri katika uhusiano baina ya Israel na Ujerumani ni muhimu kutekeleza wajibu wa kuhadithia historia juu ya wahanga na walionusurika maangamizi yaliyofanywa na mafashisti wa kijerumani.
Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri/Othman Miraji,