1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasemayo wahariri leo.

Abdu Said Mtullya16 Desemba 2009

Wahariri wa magazeti wawatetea askari wa Ujerumani waliopo Afghanistan.

https://p.dw.com/p/L3cB
Wanajeshi wa Ujerumani katika juhudi za kutoa mafunzo kwa polisi wa Afghanistan.Picha: dpa

Katika maoni yao leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanakebehi fedha uchinjo zilizotolewa na nchi za Ulaya kwa ajili ya kuzisaidia nchi masikini katika kupambana na athari za mabadiliko ya hali hewa. Wahariri hao pia wanawatetea askari wa Ujerumani wanaotekeleza jukumu la hatari nchini Afghanistan.

Hannoversche Allgemeine:

Nchi za Umoja wa Ulaya zimeahidi kutoa kiasi cha Euro bilioni 2.4 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kuzisaidia nchi masikini katika juhudi za kukabiliana na madhara yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Gazeti la Hannoversche Allgemeine linasema kiasi hicho cha fedha ni mzaha. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza:kulinganisha na fedha zilizotolewa kwa ajili ya kuyaokoa mabenki, kiasi hicho cha Euro bilioni 2.4 ni kichekesho.Mhariri huyo anasema sasa pana wasiwasi iwapo makubaliano yatafikiwa kwenye mkutano wa mjini Copengahen.

Hatahivyo ameeleza matumani juu ya kufikiwa, angalau makubaliano ya muda. Lakini jambo muhimu ni kwa nchi tajiri na zinazoinukia kukubali kuweka malengo katika kupunguza gesi chafu na kutenga fedha zaidi kwa ajili ya nchi masikini ili kuziwezesha nchi hizo kukabiliana na madhara yanatokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Bild -Zeitung:

Katika maoni yake leo gazeti la Bild-Zeitung linawatetea askari wa Ujerumani wanaotekeleza jukumu la kulinda amani na kuijenga Afghanistan. Lakini askari hao wanazungumziwa katika namna isiyofaa.Gazeti hilo linasema askari hao wanaghadhabishwa juu ya jinsi wanavyozungumziwa. Na kwa kweli wana haki ya kukasirika. Mhariri wa gazeti la Bild-Zeitung anakumbusha kwamba tokea mwaka 2001 maalfu ya wanajeshi wa Ujerumani wamekuwapo nchini Afghanistan, na 36 tayari wameshauawa.

Mhariri anasema askari hao siyo kunguru woga, na wala siyo wauaji wa raia. Wanachojaribu kufanya ni kutekeleza jukumu lao ambalo ,limezidi kuwa la hatari .Mhariri anatamka kuwa, siyo kosa la wanajeshi hao kwamba wanasiasa wanabishana juu ya istilahi za kuelezea jukumu la askari hao, iwapo wapo vitani ama la.

Hatahivyo gazeti linatamka kwamba askari hao wapo vitani, na watu nyumbani -yaani nchini Ujerumani wanapaswa kutambua hilo.

Südwest Presse:

Suala jingine lililozingatiwa na magazeti ya Ujerumani leo ni ulevi wa kupindukia miongoni mwa vijana. Juu ya tatizo hilo mhariri wa gazeti la Südwest Presse anasikitika kwa kusema kwamba idadi ya vijana wanaolewa hadi kufikia hatua ya kupoteza fahamu inaongezeka nchini Ujerumani. Vijana hao wanalewa mpaka madaktari au polisi wanaitwa , wanapokuwa kwenye "party" yaani tafrija. Gazeti linasema hiyo ni dalili ya muflisi wa maadili. Mhariri anasikitika kwamba madhumuni ya tafrija siyo tena kujenga uhusiano wa kijamii bali ni kujilipua akili.

Mwandishi/Mtullya /deutsche Zeitungen