1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti 21.12.2017

Zainab Aziz
21 Desemba 2017

Katika uchambuzi wa magazeti wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni juu ya uamuzi wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya kuhusu kuichukulia Poland hatua na juu ya mageuzi ya sheria ya kodi huko nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/2pkjl
USA - Präsident Trump - Jahresrückblick
Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imechukua hatua sahihi kwa kuuanzisha mchakato wa kuiadhibu Poland, sababu ni kwamba serikali ya chama cha kihafidhina ya nchi hiyo imepitisha mageuzi katika mfumo wa sheria ambayo kwa mtazamo wa Umoja wa Ulaya yanahujumu demokrasia. Hata hivyo waziri mkuu wa Poland amesema nchi yake haipaswi kuomba ruhusa kutoka Umoja huo ili ifanye mabadiliko kwenye mhimili wake wa mahakama. Mhariri anaendelea, anayosema waziri mkuu huyo ni sawa kabisa kwamba Poland ni nchi huru lakini anapaswa kuzingatia kuwa nchi yake ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya na hivyo ni lazima iyafuate maadili ya msingi ya Umoja huo.

Süddeutsche Zeitung

Mhariri anakumbusha kwamba Halmashauri ya Umoja wa Ulaya ilichukua muda wa miaka miwili kabla ya kupitisha uamuzi wa kuiadhibu Poland mhariri huyo anaeleza kuwa uamuzi huo wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya haukuwa rahisi kwa sababu wote wanayajua matokeo yake. Umoja wa Ulaya hautavumilia kuona mwanachama wake akiuvunja msingi wa Umoja huo. Jumuiya hiyo inafanya kazi kwa sababu wanachama wake wote wanafuata sheria sawa.

Nalo gazeti la Berliner linahoji kwamba uwezekano wa Poland kuadhibiwa ni mdogo na linafafanua kwamba serikali ya Hungary ambayo pia inakusudia kuchukua hatua kama za Poland imeshasema kwamba haitaunga mkono kutengwa kwa nchi ndugu ya Poland, ndio kusema kwa sasa hakuna kitakachofanyika dhidi ya nchi hiyo na kwa hivyo serikali ya Poland inaweza kuendelea kuwa na utulivu.

Handelsblatt

Nchini Marekani wabunge wa chama cha Republican wameyapitisha mageuzi ya sheria ya kodi yaliyopendekezwa na rais Donald Trump, mhariri wa gazeti la Handelsblatt ameandika kwamba mpaka sasa, Marekani imekuwa inatumia mfumo wa kodi usio na uhakika na wakati mwingine haukuwa katika msingi wa hali halisi kutokana na kiwango cha kodi cha asilimia 35 na ambao athari zake zilikuwa kubwa. Kutokana na kiwango hicho makampuni mengi yalikuwa hayalipi kodi na yale ya nje yalikuwa hayapeleki fedha nchini Marekani na hivyo kuisababishia hasara wizara ya fedha.

Kwa mujibu wa benki ya Goldman Sachs makampuni hayo yamelundika zaidi ya dola trilioni 2.5 katika nchi za nje ambako viwango vya kodi ni vya chini kwa hiyo manufaa ya mageuzi ya sheria ya kodi yataoneka dhahiri nchini Marekani. Wajasiriamali watawekeza zaidi nchini humo na hivyo kutenga nafasi za ajira. Naye mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine anayaona mageuzi hayo kuwa ni ya manufaa kwa Marekani na anasema lengo la mageuzi hayo ya kodi ni kusaidia uchumi wa nchi na kuiwezesha Marekani kuwa na ushindani bora zaidi katika ngazi ya kimataifa.

Hata hivyo mhariri wa gazeti la Nürnberger Nachrichten hakubaliani na hayo. Mhariri huyo anatabiri kwamba mageuzi ya kodi nchini Marekani yatatifua mawimbi ya taharuki duniani kote na kufuatiwa na ushindani wa kupunguza kodi hadi kufikia kiwango cha chini.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Yusuf Saumu