1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya ziara ya Obama, Mashariki ya Kati

Abdu Said Mtullya21 Machi 2013

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni juu ya ziara ya Rais Obama katika Mashariki ya Kati kwa kukumbusha hotuba ya matumaini aliyoitoa mjini Cairo miaka miine iliyopita

https://p.dw.com/p/181Ce
Obama na Abbas mjini Ramallah
Obama na Abbas mjini RamallahPicha: Reuters

Gazeti la "Westfälische Nachrichten" linasema katika siku ya kwanza ya ziara hiyo Rais Obama alifanya kila alichoweza ili kuondoa hisia kwamba mgogoro wa Mashariki ya Kati upo kando ya ajenda  zake muhimu.Lakini bado pana mashaka.Tokea hotuba yake ya mjini Cairo Obama bado anaandamwa na hisia kwamba anafanya juhudi za kuleta maridhiano na dunia ya kiislamu kwa kuidhuru Israel. Lakini mhariri wa gazeti la "Westfälische Nachrichten" anasema Wapalestina pia wamefadhahishwa na Rais huyo.

Mtamauko mkubwa juu ya Obama :
Mhariri wa "Nordwest"-pia anatilia maanani hisia za mtamauko juu ya  ziara ya Rais Obama katika Mashariki ya Kati.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa Waisraeli wengi wanayainua mabega yao juu ,kwa sababu Obama anaitembelea nchi yao miaka minne baada ya kuingia Ikulu.Wanamwangalia kwa nyuso za kisirani ,kwa sababu hakukabiliani na siasa ya Israel ya kuendelea kujenga makaazi ya walowezi katika maeneo ya Wapalestina.

Naye mhariri wa"Neue Osnabrücker "anakumbusha juu ya matumaini ambayo Obama aliwapa watu juu ya kuutatua mgogoro wa Mashariki ya kati.

Mhariri huyo anaeleza kwamba kauli za Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu zinaudhi,hasa kwa kutambua kwamba ujenzi wa makaazi ya walowezi unaendelea   katika sehemu ambako nchi ya Wapalestina ilipaswa kujengwa.Lingekuwa jambo la manufaa iwapo Obama angelichukua hatua za kuyafufua mazungumzo baina ya Israeli na Wapalestina.Lakini badala yake Obama amezungumzia juu mshikamano usiotetereka baina ya Marekani na Israel.Mtazamo huo unakasirisha hasa mtu akikumbuka hotuba ya matumaini makubwa aliyoitoa mjini Cairo.Mtamauko pia ni mkubwa miongoni mwa Wapalestina.

Mshikamano madhubuti:

Jee safari yote ya Obama,ina lengo la kusisitiza tu, uhusiano madhubuti baina ya Marekani na Israel? Hilo ni swali la mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" Mhariri huyo anaeleza:

Ni wazi kwamba masuala ya mgogoro wa Syria na tishio la Iran yamezingatiwa katika ziara ya Obama.Lakini kutokana na mwito wake wa Cairo kwa Waislamu na  Waarabu kuingia katika sikio la kushoto na kutokea katika sikio la kulia,hana la kufanya zaidi ya kusisitiza mshikamano baina ya Marekani  na Israel.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman