Maoni ya wahariri juu ya uchaguzi wa Marekani | Magazetini | DW | 06.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya uchaguzi wa Marekani

Wahariri wa magazeti wanazungumzia juu ya kampeni za uchaguzi nchini Marekani na juu ya wakimbizi wa Syria. Na wanatoa maoni kuhusu Ugiriki.

Michelle Obama akihutubia kwenye mkutano mkuu wa chama cha Demokratik

Michelle Obama akihutubia kwenye mkutano mkuu wa chama cha Demokratik

Juu ya Rais Obama na kampeni za uchaguzi nchini Marekani, mhariri wa gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger"anasema mke wa Obama, Michelle alifungua dimba kwenye mkutano wa chama cha demokrats kwa kutoa hotuba ya kusisimua. Na hapo kesho Obama mwenyewe atapanda jukwaani na kujaribu kuwaambia Wamarekani wamchague tena.

Mhariri wa "Reutlinger General-Anzeiger" anasema kuhusu uwezo wa kuzungumza Obama anayo turufu ya kumpiku mshindani wake Mitt Romney anaeonekana kuwa mkavu .Lakini Obama bado hajashinda. Miaka minne iliyopita aliahidi kuleta mabadiliko nchini Marekani. Mhariri wa gazeti hilo anasema mambo mengi katika maisha ya Wamarekani bado hayajabilika. Na jana tu kila mtu alipata habari kwamba Marekani ina deni la dola Trilioni 16.

Gazeti la "Braunschweiger" pia linatilia maanani kwamba wakati Obama anaanza kuimarisha kampeni ya uchaguzi, deni la Marekani limeshavuka dola Trilioni 16.

Na mhariri wa gazeti la "Delmenhorster Kreisblatt"anasema kilichobakia kwa Wamarekani sasa ni kuchagua kati ya ndwele na maradhi. Mhariri huyo anaeleza kuwa kwingineko duniani ambako Obama bado ni maarufu kama mwanamuziki ,watu wangelimchagua. Lakini kwa bahati mbaya ndani ya Marekani,vichwa vya wapiga kura vinachemka kwa namna tafauti.

Tatizo la wakimbizi linaendelea kuwa kubwa nchini Syria na sasa limefikia kiwango cha maafa. Kutokana na hali hiyo gazeti la "Stuttgarter "linaitaka serikali ya Ujerumani ifikirie juu ya kuwachukua wakimbizi zaidi kutoka sehemu za migogoro. Mhariri wa gazeti hilo anasema ni kweli kwamba Ujerumani imeshatoa Euro Milioni 22 kwa ajili ya wakimbizi wa Syria. Lakini Ujerumani haiwezi kutoa fedha tu na kujiweka kando. Jambo muhimu zaidi ni kutoa hifadhi, nchini Ujerumani, kwa idadi maalumu ya watu wanaosibika na dhiki katika sehemu za migogoro. Ni vizuri kuwahifadhi watu hao nchini Ujerumani hadi hali itakaporejea kuwa nzuri katika nchi zao.

Gazeti la "Süddeutsche" linatoa maoni juu ya mgogoro wa madeni nchini Ugiriki kwa kusema kwamba Ugiriki inapaswa kuendelea na hatua za mageuzi. Nchi hiyo lazima iendelee kubana matumizi. Lakini katika sekta zinazostahili. Kwa mfano, ni vizuri kupunguza urasimu. Kupunguza dola na kuimarisha uchumi .Lakini mpaka sasa hatua hizo hazijachukuliwa. Benki Kuu ya Ulaya sasa inapaswa kuuliza kwa nini fedha ilizotoa kwa Ugiriki haziingii katika sekta ya uchumi halisi.?

Mwandishi:Mtullya abdu/Deusche Zeitungen/

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman