1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya mshuko wa uchumi barani Ulaya,na juu ya Syria

Wahariri wanatoa maoni juu ya mshuko wa uchumi katika Ukanda wa sarafu ya Euro, na juu ya dhima ya Ulaya katika mgogoro wa Syria.Ufuatao ni muhtasari wa maoni hayo

Uchumi wa Ufaransa washuka,wananchi waandamana kupinga sera za kubana matumizi

Uchumi wa Ufaransa washuka, wananchi waandamana kupinga sera za kubana matumizi

Juu ya mshuko wa uchumi barani Ulaya gazeti la "Landeszeitung"  linaitaka   Ujerumani ilijibu swali, jee bara la Ulaya  na sarafu  ya Euro zina thamani gani  kwake.?

Ujerumani yatengwa:

Mhariri wa "Landeszeitung" anakumbusha kwamba Waziri wa fedha wa Ujerumani aliwahi kuzungumzia juu ya alichokiita kiini cha Ulaya.Yaani Ujerumani na Ufaransa ziongoze katika juhudi za kuleta Utangamano wa Ulaya.Lakini ,sasa baada ya miaka 19 Ujerumani imesimama peke yake-imetengwa, na Umoja wa Ulaya nao  umesimama njia panda.

Mhariri wa gazeti la "Landeszeitung" anasema hakuna kinachouonyesha wazi mwelekeo huo wa hatari kama ustawi wa uchumi, japo mdogo uliofikiwa Ujerumani- wakati nchi nyingine za Ukanda wa sarafu ya  Euro ,zimo katika mdororo wa uchumi na zinaipa kisogo Ujerumani. Kutokana na hali hiyo Ujerumani inapaswa kuitekeleza dhima ya kuubadilisha mwelekeo huo wa hatari.

Dhima ya Magharibi katika mgogoro wa Syria:

Gazeti la "Rheinpfalz" linazungumzia juu ya dhima ya nchi za magharibi katika  mgogoro wa Syria.

Gazeti hilo linaeleza kuwa taifa kuu duniani,Marekani,ambalo sasa limechoka, lingelifurahi, laiti lisingelihusika na mgogoro wa Syria. Inaweza kueleweka, kwa kutambua kwamba Marekani sasa, hatua kwa hatua, inamalizana na Afghanistan  baada ya kuondoka Irak. Lakini hilo haliwezekani kwa sababu nchini Syria,majeshi ya Assad yanaendelea kuwaangamiza wananchi .

Mgogoro wa Syria unazihusu Uturuki,Israel na Marekani. Ndiyo Marekani inasaidia kwa njia ya shirika lake la ujasusi,CIA na pia inasaidia kwa kuziuzia silaha, Saudi  Arabia na Katari zinazopelekwa kwa waasi. Lakini sera hiyo dhaifu inachangia  katika kukwama kwa waasi katika uwanja wa mapambano.

Waziri Mkuu Erdogan:

Mhariri wa gazeti la "Berliner Zeitung"anasema katika maoni yake kwamba siasa za Uturuki juu ya Syria zimegonga mwamba kutokana na sababu kadhaa.

Kwanza Waziri Mkuu Erdogan alitaka kuzuia kuundwa kwa sehemu ya Wakurdi yenye mamlaka ya ndani ya kujitawala.Pili Erdogan anawaunga mkono waasi wa kisuni kwa sababu za kidini ili Uturuki iweze kuwa na ushawishi, lakini katika vita vya wenyewe kwa wenyewe wanaoshinda mara nyingi ni makundi yenye itikadi kali.

Ndoto ya Erdogan ya kuwa na ushawishi nchini Syria kwa njia ya Wasuni,inaingia  giza kutokana na ukweli kwamba fedha zinazotolewa kwa ajili ya kuwasaidia waasi  wa Syria zinatoka Saudi Arabia na Katari.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri:M.Abdul-Rahman