Maoni ya wahariri juu ya kodi ya kimataifa katika sekta ya fedha. | Magazetini | DW | 19.05.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya kodi ya kimataifa katika sekta ya fedha.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya kodi ya kimataifa ya kuwabana walanguzi.

default

Soko la hisa, Frankfurt.

Serikali ya mseto ya Ujerumani imekubaliana juu ya haja ya kuanzisha utaratibu wa kodi ya shughuli zinazofanyika kwenye masoko ya hisa.

Lengo ni kusadia kudhibiti athari zinazotokana na mgogoro wa fedha duniani.Kwe usemi mwingine miamala yote inayofanyika kwenye masoko hayo itatozwa kodi . Juu ya kodi hiyo gazeti la Badische Neueste Nachrichten linasema hatimaye sasa umefika wakati wa kuwawajibisha kubeba gharama za mgogoro wa fedha, wale wanaonufaika na ununuani na uuzaji wa hisa.

Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema, kodi hiyo pekee haitazuia shughuli za ulanguzi. Sababu ni kwamba kodi hiyo haitapiga vita chanzo cha migogoro, yaani biashara inayofanyika katika misingi isiyokuwa ya busara.

Gazeti la Westdeutsche pia linaitilia mashaka kodi hiyo ya kimataifa iwapo, kweli italeta mafanikio katika juhudi za kuzuia migogoro ya fedha. Gazeti hilo linaeleza kuwa ni jambo linalostahili pongezi, kuwachukulia hatua walanguzi. Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema iwapo kodi hiyo itaweza kuzuia migogoro mingine haijulikani.Mhariri wa Westdeutsche anaeleza kuwa kodi hiyo haitakuwa nzito kiasi cha kuwakandamiza walanguzi na wamiliki wa mabenki, na hatimaye ni walipa kodi watakaobeba gharama.

Mhariri wa gazeti la Landeszeitung anaunga mkono utaratibu wa kuanzisha kodi katika biashara ya fedha ya kimataifa. Mhariri huyo anasema kodi hiyo ni hatua inayoelekea kwenye lengo sahihi.Gazeti hilo linahoji kuwa, siyo muhimu jinsi kodi hiyo itakavyoitwa; la muhimu ni kwamba wale wanaosababisha migogoro mikubwa ya fedha nao pia wabebeshwe mzigo wa gharama.

Wasichana wawili wa kijerumani waliotekwa nyara nchini Yemen wamekombolewa baada ya kuwamo katika mikono ya wateka nyara kwa muda wa karibu mwaka mmoja. Wasichana hao walitekwa nyara pamoja na wazazi wao.

Juu ya mkasa huo gazeti la Neue Osnabrücker linasema labda watu nchini Ujerumani wamepigwa butaa. Kwani inakuaje mzazi anawaingiza watoto wake katika hatari.? Hasa kwa kutambua kwamba mzazi huyo alikuwa anajaribu kueneza ukristo katika nchi kama Yemen inayofuata misingi ya dini ya kiislamu bila ya kugeuka kulia au kushoto.Hata hivyo mhariri huyo anasema kuwa siyo dhambi,kueneza neno la Biblia, bali wenye dhambi ni wale wanaoziteka nyara familia zenye watoto wadogo.Gazeti linatilia maanani kwamba serikali ya Yemen inakusudia kupambana na wanaitikadi kali. Na katika hilo, serikali ya Ujerumani inapaswa kusimama pamoja na Yemen.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri/.Abdul-Rahman