1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni juu ya mapatano ya mradi wa Nuklia wa Iran

18 Mei 2010

Iran imefikia mapatano ya kurutubishwa nje uranium

https://p.dw.com/p/NQlV
Mahmud Ahmadinedjad aregeza kamba ?Picha: AP

Waziri-mkuu wa Israel , Benjamin Netanyahu, ameitisha leo kikao maalumu na washauri wake wakuu ili kushauriana nao juu ya mapatano yaliofikiwa jana kati ya Uturuki na Brazil upande mmoja na Iran upande wapili ambayo yaweza kuzima vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa ambavyo Israel na washirika wake wamepania kuiwekea Iran.

Wakati Ikulu ya Marekani, imearifu jana kuwa juhudi za kuiwekea Iran vikwazo hivyo zinaendelea ,Waziri wa nje wa Uturuki,amedai kuregeza kamba kwa Iran kuitikiwe. rais Medvedev wa Urusi nae huku akidurusu mapatano ya jana amesema kuna swali moja la kimsingi kuulizwa: Je, Iran,itaendelea kurutubisha binafsi madini yake ya Uranium ?

ISRAEL NA KIKAO CHA DHARURA

Kikao hicho cha dharura cha Baraza la ndani la mawaziri,kimefuuatana na tangazo kutoka afisi ya waziri mkuu Netanyahu kuwa mawaziri wamepewa amri ya kutotoa matamshi yoyte hadharani na hii yabainisha wasi wasi wa Israel ilionao juu ya juhudi za nchi za nje za kupatana na Iran.Israel, inayoaminiwa kumiliki binafsi boma la silaha za nuklia,imeashiria kuichukulia Iran hatua ya kijeshi kama jaribio la mwisho kuinyima Iran, hasimu wake mkubwa uwezo wa kuunda bomu la nuklia.

Dola kuu ulimwenguni, zimeelezea shaka shaka iwapo mapatano iliofikia Iran na Brazil na Uturuki hapo jana kusafirisha sehemu ya madini ya uranium isiorutubishwa kwa kiasi kikubwa nchini Uturuki,kutatosha kuondoa kabisa wasi wasi wao kuhusu Iran ,kuendelea zaidi na kazi ya kurutubisha madini binafsi.

IRAN -MRADI WA AMANI:

Iran, inayoshikilia kudai kwamba, mradi wake wa nuklia ni wa amani ,imesema mapatano ya jana yana shabaha ya kuzima duru ya 4 ya kuwekewa vikwazo na Baraza la Usalama la UM.

Taarifa kutoka Washington ,lakini, zinasema serikali ya Marekani inahisi hatua zinaendelea mbele kupitishwa azimio la UM juu ya Iran kuwekewa vikwazo.Wakati hakutaka kutaja muda maalumu vikwazo hivyo vitawekwa, msemaji wa ikulu Robert Gibbs alisema, "Nadhani tunapiga hatua sawa kuelekea kupitisha azimio la vikwazo."

Taarifa ya kwanza ya kufikiwa muwafaka iliotolewa na Brazil na Uturuki,zote mbili si wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ,ilisababisha muitikio tofauti kutoka kwa maafisa wa Israel waliozungumza na vyombo vya habari kabla kunyamazishwa na waziri mkuu Netanyahu.

Rais Dimitry Medvedev wa Urusi, amesema kwamba, anayadurusu mapatano ya jana lakini, kuna swali moja : "Je, Iran binafsi itarutubisha madini yake ya uranium ? " Rais Medvedev, akaongeza kusema kwamba, kwa kadri anavyoelewa yeye kutoka wakuu wa Iran, shughuli hiyo itaendelea.

MSIMAMO WA CHINA:

China, ambayop kama Urusi, ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la UM, imekaribisha mapatano ya jana ya mradi wa nuklia wa Iran; na imetaka mazungumzo juu ya mzozo huu unaozidi kati ya Iran na Kambi ya magharibi, yafanyike hata ikiwa dola za magharibi, zimeyalaani mapatano hayo mapya.Waziri wa nje wa Uturuki,amesema Iran , kwa kuridhia kusafirisha madini yake nje kurutubishwa,kumebainisha kuregeza kwake kamba na nia yake njema ya kisiasa na kwamba, iitikiwe kwa kutatua mgogoro huu kidiplomasia.

Mwandishi: RamadhanAli/RTRE/APE

Uhariri: Abdul-Rahman