1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mandela afikisha miaka 93 ya kuzaliwa

18 Julai 2011

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amewataka watu duniani kote kutumia sherehe ya kuzaliwa kwa rais wa zamani wa Afrika kusini, Mzee Nelson Mandela, kwa kufanya kazi za kujitolea kama Mandela mwenyewe.

https://p.dw.com/p/RaTj
Nelson Mandela na mkewe Graca Machel
Nelson Mandela na mkewe Graca MachelPicha: AP

Katika ujumbe wake alioutoa kwa njia ya video, Ban Ki-moon ameelezea njia mbalimbali za kuenzi kazi alizozifanya kiongozi huyo, ikiwemo kufundisha watoto, kujali mazingira, kusaidia wasiojiweza na kushiriki kazi za kujitolea mahospitalini na katika vituo vya kijamii.

Wakfu wa Nelson Mandela na Umoja wa Mataifa pia umewataka watu kutumia dakika 67 kwa kazi za kujitolea katika kumuenzi mwanasiasa huyo.

Umoja wa Mataifa umeitambua Julai 18, tarehe na mwezi aliozaliwa Mzee Mandela kama siku ambayo watu wanatolewa wito kujitolea katika jamii zao na inajulikana kama Siku ya Mandela.

Katika kuadhimisha siku hii, leo nchini Afrika Kusini kwenyewe takribani wanafunzi milioni 12.4 wa shule wataimba wimbo maalumu wa kumtakia kheri za kuzaliwa Mzee Mandela.

Mapigano yapamba moto Brega

Majeruhi wa mapigano ya Libya
Majeruhi wa mapigano ya LibyaPicha: dapd

Mapambano makali kuuwania mji wenye utajiri wa mafuta wa Brega bado yanaendelea nchini Libya kati ya waasi na vikosi vitiifu kwa kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi.

Msemaji wa waasi, Mohammed Zawi, amesema licha ya kufanikiwa kuingia katika mji huo, bado hawajafanikiwa kuudhibiti wote kutoka kwa wanajeshi wa Gaddafi.

Tangu mapigano kuupigani mji huo yaanze Alhamisi iliyopita, jumla ya wapiganaji 15 wameuawa na wengine 274 wamejeruhiwa.

Wakati mapigano hayo yakiendelea mjini Brega, mfululizo wa miripuko imesikika katika mji mkuu wa Tripoli, baada ya Gaddafi kuapa kwamba kamwe hatajiuzulu na hatokimbilia uhamishoni.

Cameron yuko Afrika ya Kusini

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron
Waziri Mkuu wa Uingereza, David CameronPicha: picture alliance / empics

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, leo anaanza ziara ya kibiashara ya siku mbili barani Afrika, kituo chake cha kwanza kikiwa Afrika kusini.

Katika ziara hiyo, Cameron ameambatana na ujumbe wa wafanyabiashara wa ngazi ya juu.

Hata hivyo, ziara hiyo imefupishwa kutokana na kashfa ya unasaji mazungumzo ya simu, ambayo imesababisha Kamishna wa polisi wa mjini London, Paul Stephenson, kujiuzulu.

Awali ziara hiyo ilipangwa iwe ya siku tano, ambapo pia angelitembelea taifa jipya la Sudan Kusini na Rwanda.

Akiwa nchini Afrika Kusini, Waziri mkuu wa Uingereza, ambaye amelitolea wito bara la Afrika kuimarisha biashara ndani ya bara hilo ili kupunguza kutegemea misaada, anatarajia kufanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma, pamoja na mwanaharakati, Askofu Desmond Tutu.

Hii ni ziara ya kwanza kwa Camron kulitembelea eneo la kusini mwa jangwa la Sahara tangu alipoingia madarakani mwaka 2010.

Ujerumani kuongeza msaada kwa wahanga wa njaa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido WesterwellePicha: picture alliance/dpa

Mawaziri wa Mambo ya Kigeni na wa Ushirkiano wa Kiuchumi wa Ujerumani, Guido Westerwelle na Dirk Niebel, wameelezea kuingiwa na wasiwasi juu ya maafa ya njaa na ya kiutu katika eneo la Pembe ya Afrika.

Wamesema wasiwasi wao hasa unaelekezwa juu ya wanawake na watoto ambao wameathirika kutokana na ukame na mizozo ilioko huko Somalia.

Kwa hivyo, serekali ya Ujerumani imeongeza kwa haraka msaada wake kwa Euro milioni tano. Pia mawaziri hao wametoa mwito kwa wananchi wa Ujerumani wawe tayari kuchangia ili kuwasidia watu wa maeneo hayo yalioathrika, kwani jumuiya za Ujerumani za kutoa misaada zina uhakika ya kufikisha misaada hiyo kwa watu walioathirika.

Fedha ambazo zimeshatolewa, nusu kwa nusu baina ya Wizara ya Mambo ya Kigeni na ile ya Ushirkiano wa Kiuchumi, zitatumiwa kuwasaidia wakimbizi, watu waliopoteza makaazi ndani ya nchi, pia wanawake na watoto walioko katika maeneo yalioathirika watapatiwa mahitaji ya dharura.

Maafa ya kibinaadamu katika maeneo makubwa ya Somalia, Kenya, Ethiopia, Eritrea na Djibout yameongezeka katika wiki zilizopita, ambapo ukame uliolikumba eneo hilo umesababisha ukosefu wa mazao ya shambani na kupanda kwa bei za vyakula.

Katika mwaka 2011, Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ujerumani ilitoa Euro milioni 3.6 kwa misaada ya kiutu katika eneo la Pembe ya Afrika.