Mandela aadhimisha miaka 94 tangu kuzaliwa | Matukio ya Afrika | DW | 18.07.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Mandela aadhimisha miaka 94 tangu kuzaliwa

Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Madiba Mandela, ametumia maadhimisho ya sherehe za kuzaliwa kwake akiutaka ulimwengu kumuenzi kwa kujitolea kwa shughuli za kijamii.

Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini, Mzee Nelson Mandela.

Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini, Mzee Nelson Mandela.

Kiongozi huyo anayetimiza leo miaka 94, yuko katika kijii alichozaliwa cha Qunu kwenye jimbo la Cape ya Mashariki anakoishi baada ya kustaafu kwake siasa.

Wakati wa hafla hiyo takriban wanafunzi milioni 12 nchini kote wameimba wimbo maalum wa kumpongeza kwa kufikisha miaka 94 ya uhai wake, huku wakisema "Tunakupenda baba."

Mmoja wa wanafunzi hao, msichana wa miaka 12 katika shule ya msingi ya Soweto, Kgaugelo Mashunhloane, alisema wanasherekea siku ya kuzaliwa kwa Mandela, anayefahamika zaidi kwa jina la kwao la Madiba, "huku tukikumbuka namna alivyopigania uhuru wetu, alipigania dhidi ubaguzi wa rangi katika taifa letu."

Mzee Mandela ameadhimisha siku yake ya kuzaliwa akiwa na familia yake na marafiki huku shughuli mbalimbali zikiandaliwa nchini humo na makundi mbali mbali ikiwa ni ishara ya kumpa heshima, wakitambua juhudi zake za kupigania uhuru wa taifa hilo lilolokuwa likiongozwa rasmi na ubaguzi wa rangi.

Sherehe na familia yake tu

Nelson Mandela akiwa kijana mwaka 1964.

Nelson Mandela akiwa kijana mwaka 1964.

Kwa miaka ya hivi karibuni, Mzee Mandela amekuwa akijiepusha kujitokeza hadharani, ambapo amekuwa akitumia muda wake zaidi kukaa na familia nyumbani kwake katika kijiji cha Qunu. Mara ya mwisho kuonekana hadharani, ilikuwa ni wakati wa sherehe za kufunga michezo ya kombe la dunia katika mji mkuu wa nchi hiyo, Johannesberg mwaka 2010.

Awali, mjukuu wake, Ndileka Mandela aliviambia vyombo vya habari nchini humo kuwa familia itaadhimisha sherehe hizo kwa kula chakula maalum kwa pamoja, chakula ambacho hupendwa na rais huyo wa zamani sambamba na kukata keki.

Obama, Clinton wampongeza Mandela

Nelson Mandela na Bill Clinton ndani ya gereza ka kisiwa cha Robben.

Nelson Mandela na Bill Clinton ndani ya gereza ka kisiwa cha Robben.

Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton alimtembelea Mzee Mandela nyumbani kwake Qunu na kusalimiana naye.

"Nikitafakari aliyoyafanya Mzee Mandela naona kwamba ni mtu aliyejitolea kuangalia zaidi mbele", alisema Rais Clinton alipokuwa akiondoka nyumbani kwa Mzee Mandela na kusisitiza kuwa wawili hao walifanya kazi pamoja wakiwa marais na hata baada ya kuondoka kwao madarakani. "Tuliendelea kufanya kazi kwa pamoja katika kuboresha mfumo wa elimu kwa wanafunzi duniani ili kuwa na taifa lenye kufikiria mbele."

Rais Barack Obama na mke wake Michelle wamemwelezea Mzee Mandela kama mtu ambaye dunia itaendelea kumuheshimu kutokana na ujasiri wake na kuendelea kudumisha misingi ya demokrasia yenye kujali utu, haki na uhuru.

Siku ya kuzaliwa kwake pia inaadhimishwa na Umoja wa Mataifa kutokana na mchango wake katika kuikomboa Afrika Kusini dhidi ya utawala wa kikaburu.

Mzee Mandela aliachiliwa huru kutoka gerezani alikokaa kwa miaka 27 akiwa na umri wa miaka 67 na alichaguliwa kuwa rais wa Afrika Kusini mwaka wa 1994.

Mwandishi: Flora Nzema/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef