1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malengo ya Milenia yatatimizwa kwa wakati?

P.Martin17 Septemba 2007

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linakutana mjini New York leo Jumanne.Miaka saba iliyopita,madola ya kimataifa yalikubaliana kuhusu malengo manane yaliyoitwa „Malengo ya Milenia.“

https://p.dw.com/p/CB18

Wanachama wa Umoja wa Mataifa walipokubaliana na malengo ya milenia katika mwaka 2000,hilo lilikuwa tangazo la nia lililotolewa mwanzoni mwa milenia mpya.Viongozi hao walisema:umasikini upunguzwe kwa nusu kote duniani,watoto wote wapatiwe elimu,uwepo usawa wa kijinsia,idadi ya vifo vya watoto na akina mama ipunguzwe,magonjwa kama UKIMWI na malaria yapigwe vita,mazingira yahifadhiwe na uwepo ushirikiano kati ya nchi tajiri na zilizo masikini.

Wakati huo,hakuna hata nchi moja iliyodhani kuwa itashinikizwa kutimiza ahadi hizo.Lakini baada ya kuwepo shaka fulani hapo mwanzoni,katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2005,kila alietia saini makubaliano hayo,alielewa kuwa haiwezekani tena kujiepusha na malengo yaliyowekwa.

Kwa maoni ya Mratibu wa Malengo ya Milenia wa Umoja wa Mataifa,Bibi Eveline Herfkens,tayari yapo masharti ya mwanzo.

Vile vile kwa mara ya kwanza,ule msimamo wa kuwa kama nahodha umebadilika kuwa ujumbe wa ushirikiano.Kwa maoni yake,msimamo wa hapo awali,si ujinga tu bali ni kikwazo kuamini kwamba nchi zinaweza kufanyiwa maendeleo kutoka nje.Anasema,somo kubwa lililopatikana baada ya kutolewa misaada ya maendeleo kwa muda wa miaka 40 hadi 50 ni kwamba nchi fadhila kwa miradi na mahitajio yake,zimeathiri uwezo wa nchi masikini kujiwajibisha kwa maendeleo yake.Nchi hizo zimepoteza rasli mali na wakati mwingi kulipa madeni hadi kufikia hali ya kutowajibikia wananchi.Akaongezea:

“Malengo ya milenia hayatoweza kutekelezwa,ikiwa serikali zenyewe,hazitobeba majukumu ya nchi.Vile vile wananchi lazima waziwajibishe serikali hizo.“

Licha ya kuwepo masharti ya mwanzo,kutekeleza malengo ya milenia,mafanikio yaliyopatikana baada ya miaka mitano yanashtusha.Kuna nchi ambako malengo hayo yatatekelezwa,lakini ukweli ni kwamba nchi nyingi huenda zikatimiza malengo mawili au matatu kutoka jumla ya malengo manane yaliyowekwa mwanzoni wa milenia mpya.