1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malala akutana na Rais Goodluck Jonathan

Mjahida14 Julai 2014

Mwanaharakati anayepigania haki ya elimu kwa wasichana Malala Yousafzai anasheherekea siku yake ya kuzaliwa Nigeria kwa kukutana na Rais Goodluck Jonathan na wazazi wa wasichana zaidi ya 200 wanaozuiliwa na Boko Haram

https://p.dw.com/p/1Ccki
Mwanaharakati anayepigania haki ya elimu kwa wasichana Malala Yousafzai
Mwanaharakati anayepigania haki ya elimu kwa wasichana Malala YousafzaiPicha: Screenshot Twitter

Malala Yousafzai, raia wa Pakistani, amesema kile anachokiomba na kukitaka kwa siku yake ya kuzaliwa ni wasichana hao warejee nyumbani haraka na wakiwa hai. Msichana huyo aliyenusurika jaribio la kumuua lililofanywa na wanamgambo wa Taliban, kwa kumpiga risasi kichwani, wakati alipokuwa anatoka shuleni nchini Pakistan mwaka wa 2012, amekutana na rais Goodluck Jonathan mjini Abuja hii leo.

"Nimezungumza naye kuhusu wale wasichana niliokutana nao jana walioniambiya, hawawezi kwenda shule, wana ndoto ya kuwa madaktari wahandisi na walimu lakini serikali haifanyi lolote kutimiza ndoto zao, wanahitaji usalama kwa hivyo nimemueleza rais, hizi ndizo shida dada zangu wanazokumbana nazo kwa kuhofia kutekwa na Boko Haram," Alisema Malala.

Ameongeza kuwa rais Goodluck Jonathan amemuahidi kulishughulikia suala hilo na hata kuahidi kwamba watoto waliotekwa watarejea nyumbani haraka iwezekanavyo.

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan
Rais wa Nigeria Goodluck JonathanPicha: imago/Wolf P. Prange

Hadi sasa Rais Jonathan hajakutana na wazazi wa wasichana waliotekwa, wale walioachiwa au wanaharakati walioanzisha vuguvugu la kampeni Bring Back Our Girls, warejeshe nyumbani wasichana wetu.

Hatua ya Jonathan imelaaniwa vikali kimataifa huku serikali ya taifa hilo la Afrika Magharibi ikionekana kushindwa kuwaokoa wasichana waliotekwa miezi mitatu iliopita tangu Aprili 15, mjini Chibok.

Malala asema ataendelea na kampeni hadi wasichana waachiwe

Malala Yousafzai amesema ataendelea na kampeni hiyo hadi pale atakapoona wasichana waliotekwa wamerejea nyumbani.

"Nitahesabu siku, na nitaangalia lini wasichana hao watarejeshwa nyumbani, nitanedelea na kampeni hii hadi ntakapowaona wamerudi kwa familia zao, iwapo Nigeria inataka kuwa na hali nzuri katika siku za usoni, basi lazima kila mtoto hapa apate nafasi ya kwenda shule," Alielezea Malala Yousafzai.

Mwanaharakati huyo wa elimu kwa wasichana aliye na umri mdogo pia pia ameitaka serikali ya Nigeria kuekeza kiwango kikubwa cha fedha katika sekta ya elimu ili kupunguza idadi ya maelfu ya wasichana wanaoshindwa kwenda shule.

Malala akiwa na wajumbe wengine katika ziara yake Nigeria
Malala akiwa na wajumbe wengine katika ziara yake NigeriaPicha: Reuters

Wakati huo huo Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa itikadi kali Boko Harram, Abubakar Shekau wiki iliopita alitoa video mpya akirudia matakwa yake kwamba serikali ya Nigeria iwaachie wapiganaji wake inaowazuia, kama mpango wa kubadilishana na wasichana hao.

Mwezi Mei rais Goodluck Jonathan alifutilia mbali mipango yake ya kukitembelea kijiji cha Chibok huku wanajeshi na polisi wakiwazuwiya waandamanaji mwezi Aprili mwanzoni mwa kisa hiki, waliopanga kwenda hadi Ikulu mjini Abuja kuwasilisha madai yao.

Mwandishi Amina Abubakar/AP/Reuters

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman