1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano yafikiwa kutatuwa mzozo wa Ukraine

18 Aprili 2014

Urusi ,Ukraine na Mataifa ya Magharibi zimefikia makubaliano bila ya kutegemewa mjini Geneva Alhamisi (17.04.2014) yenye lengo la kupunguza mvutano wa mzozo wa Ukraine kati ya mataifa ya magharibi na Urusi.

https://p.dw.com/p/1BkfT
Mkutano wa pande nne kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa Ukraine Geneva.(17.04.2014)
Mkutano wa pande nne kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa Ukraine Geneva.(17.04.2014)Picha: picture-alliance/dpa

Makubaliano hayo yameainisha hatua madhubuti za kurudisha usalama kwa raia wote na kusisitiza umuhimu wa makundi yote ya watu wenye silaha kusalimisha silaha zao na kuondoka kwenye majengo wanayoyashikilia.

Makubaliano hayo hayakufafanuwa wazi wazi iwapo inakusudia watu hao kuwa ni wanaharakti wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi ambao wamechukuwa baadhi ya maeneo yenye vurugu kusini mashariki ya Ukraine.

Makubaliano hayo ni tafauti kabisa na kauli iliyotolewa na Rais Vladimir Putin iliyotolewa hapo awali ambapo aliweka wazi uwezekano wa kuingilia kati kijeshi nchini Ukraine.

Obama ana mashaka na utekelezaji

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon amesema ameshajiishwa kwamba mazungumzo hayo ya pande nne yameweza kuzaa makubaliano na kutaraji pande zote kuonyesha umakini wao katika kuyatekeleza

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir pia ameyakaribisha makubaliano hayo kama hatua ya kwanza muhimu lakini Obama ameyakaribisha kwa tahadhari kwa kusema kwamba hawatoyategemea hadi pale watakapoyaona.

Obama amewaambia waandishi wa habari kwamba kwa hivi sasa hawawezi kuwa na uhakika wa kila kitu lakini kuna uwezekano kwamba dilomasia yumkini ikapunguza hali ya kupamba moto kwa mzozo huo.

Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: DW/V. Over

Wakati huo huo Obama amesema amekuwa akiwasiliana na viongozi wa Ulaya kuhusu kuiwekea vikwazo zaidi Urusi iwapo hakutoshuhudiwa maendeleo katika siku zijazo.

Marekani na Umoja wa Ulaya tayari zimeweka vikwazo vya kuwaadhibu viongozi wakuu wa kisiasa na kibiashara wa Urusi na Ukraine wakiwemo watu walio karibu na Putin.

Tishio la Urusi

Mapema hapo jana Rais Putin wa Urusi amesema anataraji hatolazimika kutumia haki yake ya kutuma vikosi yake kwa nchi jirani kwa kile kinachoonekana kuwa ni tishio lisilo wazi kwa serikali ya Ukraine.

Amekaririwa akisema ana matumaini makubwa kwamba hatolazimika kutumia haki yake hiyo na kwamba kwa kupitia njia za kisiasa na kidiplomasia wanaweza kutatuwa matatizo yote sugu ya Ukraine na kuonya kwamba nchi hiyo inatumbukia kwenye hali ya kukata tamaa kabisa.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: Reuters/Alexei Nikolskyi/RIA Novosti

Kutokana na kupamba moto kwa mzozo huo wa Ukraine serikali ya nchi hiyo iliwapiga marufuku wanaume wote wa Urusi wenye umri wa miaka 16 hadi 60 kuingia katika ardhi ya Ukraine hatua ambayo waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema inakirihisha.

Siku moja baada ya kufikiwa kwa makubaliano kati ya Urusi na Mataifa ya magharibi mjini Geneva ya kupunguza mvutano katika jimbo hilo la zamani la muungano wa Kisovieti waasi wanaoiunga mkono Urusi leo wameendelea kuyashikilia majengo ya serikali huko Ukraine

Watu hao wenye silaha ambao wameichukuwa miji kadhaa midogo na mikubwa katika eneo la kusini mashariki mwa Ukraine lenye kuzungumza Kirusi kumekuwa hakuna dalili ya kuondoka kwenye sehemu hizo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu