Makubaliano dhidi ya silaha ndogo ndogo yatafikiwa lini? | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Makubaliano dhidi ya silaha ndogo ndogo yatafikiwa lini?

Kamati ya Umoja wa mataifa inayosimamia amani na kupunguzwa silaha inakutana mjini New-York

Jeshi la Ujerumani lateketeza silaha ndogo ndogo nchini Bosnia

Jeshi la Ujerumani lateketeza silaha ndogo ndogo nchini Bosnia


Ya kwanza kati ya kamati mbali mbali za Umoja wa mataifa ni ile inayoshughulikia usalama na kupunguza silaha-mada kuu tangu Umoja wa mataifa ulipoundwa.Kimsingi kinachoshughulikiwa hapo ni masuala ya kupunguza silaha na kuepukana na majanga ya mizozo ya kimataifa au ya kimkoa.Lakini mizozo inayoshuhudiwa enzi hizi tulizo nazo,yaani enzi za baada ya vita baridi,sio tuu mizozo kati ya mataifa na wanajeshi.Katika nchi nyingi za dunia yetu kumezuka vita vya raia wenyewe kwa wenyewe,matumizi ya nguvu na uhalifu ni mambo yanayoshuhudiwa kila kukicha.Mazungumzo yanaendelea mjini New-York wakati huu tulio nao kujaribu kufikia makubaliano ya kimataifa dhidi ya biashara ya silaha ndogo ndogo.

Silaha ndogo ndogo milioni 875 zimeenea katika kila pembe ya dunia-Robo tuu ya silaha hizo ndizo zinazodhibitiwa na vyombo vya kiserikali,polisi au wanajeshi.Kila siku,watu elfu moja wanauliwa kwa silaha ndogo ndogo:wanawake,watoto na wanaume,wasiolitumia jeshi lolote,wanajishughulisha na pirika pirika za kimaisha tuu,hadi wanapoangukia mhanga wa mojawapo wa silaha milioni 650 zilizotapakaa na kumilikiwa na watu binafsi kote ulimwenguni.

Mamoja nchi au eneo ni maskini vipi:silaha zinakutikana hata kule ambako hata chakula na maji vinakosekana.Katika kambi za wakimbizi watu wanajikuta upya wakiandamwa na matumizi ya nguvu waliyoyapa kisogo hapo awali.

Katika miji mikubwa mikubwa ambako matajiri wanashindana na maskini,na ambako mitaa ya madongo poromoka inatoa sura halisi ya ukosefu wa usawa miongoni mwa jamii,silaha ndizo zinazoamua mwenye usemi ni nani katika maisha ya kijamii.

Katika maeneo ya wahalifu,sheria zinaamuliwa kwa mtutu wa bunduki-nani anastahiki kufaidika na biashara ya wajakazi na madawa ya kulevya.Lakini hata katika maeneo wanakoishi watu wa kawaida,ambako silaha zinakutikana ili „kujihami ikilazimika“,watu pia wanauliwa kwa silaha.

Ni sawa na sheria za kimaumbile kwamba silaha zinatumiwa tuu kule zinakokutikana-naiwe kwa kuvutiwa au kwa kudhamiria,naiwe kwa sababu ya faida au kwa kisasi.Pekee biashara ya silaha ndogo ndogo itakapowekewa vizuwizi –kwa kuidhinishwa makubaliano ya kimataifa,kwa kusajiliwa silaha,kwa kuteketezwa ghala za silaha,ndipo vita vya mtu kwa mtu vitakapokoma.

Silaha laki mbili za mkononi tayari zimeshaingia kichini chini nchini Irak kutoka Bosnia.Silaha hizo zilikua sehemu ya shehena ya zamani ya Bosnia ambayo wizara ya ulinzi ya Marekani ilizidhibiti kwa lengo la kupelekewa vikosi vya usalama vya Irak.Hakuna ajuaye,silaha hizo zimepotelea wapi-lakini huhitaji kupiga ramli kuweza kutambua kwamba hazikuangukia katika mikono ya wenye imani.

Katika nchi mfano wa Irak ambako mfumo wa jamii umevurugika,matumizi ya nguvu yanashuhudiwa kila kukicha,silaha laki mbili ndogo ndogo zitazidisha bila ya shaka idadi ya wanaopoteza maisha yao.

Hali sawa na hiyo inakutikana pia nchini Kongo,Sudan au Somalia-tukiitaja mifano michache tuu.

Ikiwa Umoja wa mataifa utaharakisha ,basi makubaliano kuhusu kupunguzwa silaha ndogo ndogo yanaweza kufikiwa mwaka 2010.Mijadala imeshaanza katika kamati husika,lakini hadi pingamizi za urasimu zitakapoondolewa na mswaada wa azimio kuwasilishwa- miaka miwili au hata mitatu itapita.Na hadi mwaka 2010,watu wengine wasiopungua milioni moja na laki mbili wataangukia mhanga wa matumizi ya nguvu kwa silaha ndogo ndogo.

 • Tarehe 26.10.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/C7gF
 • Tarehe 26.10.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/C7gF

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com