Majeshi ya Kenya yaingia kwenye ardhi ya Somalia | Matukio ya Afrika | DW | 17.10.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Majeshi ya Kenya yaingia kwenye ardhi ya Somalia

Operesheni ya jeshi la Kenya dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabbaab nchini Somalia, imeanza rasmi baada ya vifaru vya mamia ya wanajeshi wa Kenya kuingia Somalia wakiwa na mizinga, vifaru na helikopta za kivita.

Wapiganaji wa Al-Shabbaab wakifanya mazoezi

Wapiganaji wa Al-Shabbaab wakifanya mazoezi

Ndege za kivita na helikopta zimekuwa zikiruka angani katika eneo hilo tokea vikosi vya Kenya vilipoanza kuingia kwa wingi nchini Somalia hapo jana.

Uvamizi huo umekuja siku moja baada ya maafisa wa ulinzi wa Kenya kusema kwamba nchi hiyo ina haki ya kujihami dhidi ya wanamgambo wa al- Shabaab kufuatia wimbi la utekaji nyara nchini Kenya. Raia wanne wa Ulaya wametekwa nyara na mmoja kuuwawa nchiuni Kenya hivi karibuni.

Mashahidi katika mji mdogo wa Dhobley nchini Somalia, wamesema leo hii magari ya kijeshi ya Kenya yanayokadiriwa kufikia 40 yaliingia katika mji huo hapo jana. Kwa mujibu wa mashahidi hao, hadi sasa hakuna mapigano makubwa yaliyozuka.

Hapo jana helikopta ya kijeshi ilianguka na kushika moto ndani ya Kenya kutokana na tatizo la kiufundi wanajeshi, ambapo watano wa Kenya wameuwawa katika ajali hiyo.

'Mamluki' waliokuwa Libya wauwa Mali

Wapiganaji nchini Libya

Wapiganaji nchini Libya

Wapiganaji wamemuuwa mwanajeshi mmoja wa Mali kaskazini mwa nchi hiyo hapo jana, katika kile kinachoelezwa kuwa mfululizo wa mashambulizi yanayolaumiwa kufanywa na wapiganaji hao wanaorudi kutoka nchi jirani ya Libya.

Kifo cha mwanajeshi huyo ni cha karibuni kabisa katika mfululizo wa mashambulizi ya kutumia silaha kaskazini mwa Mali, ambayo yamesadifu na kurudi kutoka Libya kwa mamia ya wapiganaji wa kutoka Mali waliotumika katika vikosi vya kiongozi wa Libya aliyepinduliwa madarakani, Muammar Gaddafi.

Zaidi ya watu 400 wa kabila la Tuareg nchini Mali wamewasili nchini humo kutoka Libya hapo Jumamosi, wakiwa kwenye magari 80 na kuyaacha mapigano nchini humo wakati nguvu ya vikosi vya Gaddafi zikizidi kudhoofíka.

Museveni awakingia kifua wanajeshi wa Marekani

Rais Yoweri Museveni (katikati) akikagua gwaride la heshima mjini Kampala.

Rais Yoweri Museveni (katikati) akikagua gwaride la heshima mjini Kampala.

Rais Yoweri Musevi wa Uganda amesema kwamba wanajeshi wa Marekani wanaotumwa nchini Uganda kusaidia katika mapambano dhidi ya kundi la waasi wa Lord Resistance Army (LRA) hawatoshiriki katika mapigano halisi.

Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, Rais Museveni alisema itakuwa kosa kusema kwamba Marekani inatuma wanajeshi wake kwa lengo la kupambana na kiongozi wa LRA, Joseph Kony.

Rais huyo wa Uganda amesema pia hawezi kuruhusu wanajeshi wa kigeni kuwasaidia katika vita dhidi ya LRA kwa sababu Uganda ina uwezo wa kufanya hivyo.

Rais wa Marekani, Barack Obama, Ijumaa iliyopita alitangaza kwamba atatuma kikosi cha kiasi wanajeshi 100 huko Afrika ya Kati kwa lengo la kutoa ushauri katika opresheni ya mapambano dhidi ya LRA, kundi linalotuhumiwa kuendesha mauaji ya watu katika nchi kadhaa.

Mbunge auawa Nigeria

Polisi wakiokoa wahanga wa mashambulizi ya Abuja mapema mwaka huu.

Polisi wakiokoa wahanga wa mashambulizi ya Abuja mapema mwaka huu.

Watu wanaotuhumiwa kuwa wanachama wa kundi la Kiislam wamempiga risasi na kumuuwa mbunge mmoja wa Nigeria katika mfululizo wa mashambulizi katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Mbunge huyo, Modu Bintube, aliuawa na watu wenye silaha akiwa nyumbani kwake jioni ya jana huko Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno, kwenye pembe ya kaskazini mashariki mwa Nigeria, karibu na mipaka ya Cameroon, Niger na Chad.

Msemaji wa polisi amesema mbunge huyo amepigwa risasi mbele ya nyumba yake na kwamba msako mkali unafanyika kuwatafuta wauaji wake.

Kundi la Boko Haram, ambalo jina lake linamaanisha kwamba elimu ya kimagharibi ni marufuku, limekuwa likilaumiwa na polisi kwa mauaji na mashambulizi ya kila siku kwa kutumia mabomu yaliyotengenezwa kienyeji huko Maiduguri. Katika miezi ya hivi karibuni, mara nyingi mashambulizi hayo yamekuwa yakiwalenga maafaisa wa serikali.

Polisi ya Uganda yavunja maandamano ya amani

Kiongozi wa upinzani wa Uganda, Kizya Besigye

Kiongozi wa upinzani wa Uganda, Kizya Besigye

Polisi wa Uganda leo hii wamevunja maandamano ya kupinga mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha kwa kutumia gesi na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji.

Msemaji wa polisi, Iddi Senkumbi, ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani (DPA), kwamba wamekuwa wakijaribu kurudisha utulivu, lakini watu ambao amewaita wahuni wamekuwa wakiwarushia polisi mawe na vitu vyengine.

Maduka yamefungwa katika sehemu kadhaa za mji huo, wakati mamia ya polisi wa kutuliza ghasia wakiwa wametawanywa kudhibiti machafuko hayo.

Wanafunzi 10 katika shule moja ya sekondari mjini Kampala wamekimbizwa hospitali baada ya bomu la kutoa machozi kuripuka darasani mwao, wakati wakiwa kwenye mitihani ya mwisho wa mwaka.

Maandamano ya kisiasa na fujo yamekuwa yakilitingisha taifa hilo la Afrika Mashariki mara kwa mara, tokea Rais Yoweri Museveni alipochaguliwa tena mapema mwaka huu.

Mwandishi: Mohammed Dahman/DPA/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf

 • Tarehe 17.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12tYs
 • Tarehe 17.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12tYs