1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Iraq yaanza tena mashambulizi dhidi ya IS

29 Desemba 2016

Majeshi ya Iraq yameanza awamu yake ya pili ya mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS katika moja ya ngome zake kuu katika mji wa Mosul.

https://p.dw.com/p/2V1Ca
Irak Mossul Militär
Picha: Getty Images/A.Al-Rubaye

Majeshi yanashambulia kutoka pande tatu tofauti kuingia maeneo ya Mashariki wa mji huo ambako mapigano yalikuwa yamesimama kwa karibu mwezi mmoja sasa.

Mashambulizi hayo yanalenga kukomboa sehemu ya eneo la Mashariki mwa mji wa Mosul kutoka kwa kundi la IS. Taarifa ya kamanda wa kampeni hiyo Adbul Amir Rasheed inasema kuwa, vikosi vya jeshi, askari wa shirikisho na vikosi vya kupambana na ugaidi vimeanza utekelezaji wa hatua ya pili ya oparesheni hiyo kwa lengo la kulikomboa kabisa eneo la Mashariki mwa Mosul.

Ikiwa ni wiki ya 10 sasa tangu kuanza kwa mashambulizi ya kuutwa mji wa Mosul, majeshi ambayo yanapambana na ugaidi yamefanikiwa kutwaa robo ya mji ambao ni ngome kuu ya mwisho ya kundi hilo nchini Iraq.

Kampeni hiyo ambayo ni moja kati ya oparesheni kubwa kuwahi kufanyika nchini humo baada ya ile iliyofanywa mwaka 2003 ikiongozwa na Marekani ambayo iliuondoa madarakani utawala wa Saddam Hussein, mapema mwezi huu iliingia katika hatua muhimu ya mapumziko ili kufanya maboresho na kujipanga zaidi.

Maelfu ya raia mpaka siku ya jana walikuwa wakisubiri kusafirishwa kwenda katika kambi za watu ambao hawana makaazi baada ya kukimbia makaazi yao Mashariki mwa Mosul, eneo ambalo hata hivyo limetwaliwa na jeshi karibuni. 

Irakische Leute sammeln Wasser in Mosul
Baadhi ya wakaazi wa Mosul wakisubiri kupata maji. Picha: Reuters/A. Al-Marjani

Katikati ya mwezi wa Oktoba, majeshi ya serikali yakiongozwa na muungano wa Marekani pamoja na wapiganaji wa Kikurd walianza kampeni iliyokuwa inasubiriwa kwa muda mrefu ya kuutwaa tena mji wa Mosul kutoka katika utawala wa IS, japo maendeleo ya kampeni hiyo yalidorora katika wiki za hivi karibuni kutokana na wanagambo wa IS kukabiliana na mashambulizi katika wilaya ambazo zina wakaazi wengi lakini pia kumekuwepo na hali mbaya ya hewa.

Wiki iliyopita Waziri Mkuu Haider al Abadi alisema kuwa mchakato wa kuudhibiti kamili mji wa Mosul unaweza kuchukua miezi mitatu zaidi. Kundi hilo la kigaidi linaamika kuwashikilia maelfu ya raia wa Iraq ndani na maeneo jirani ya mji wa Mosul na kuwatumia kama ngao ya mapigano.

Mosul mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq umekuwa chini ya utawala wa kundi la IS tangu katikati mwa mwaka 2014

Mwandishi: Celina Mwakabwale/DPA/Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo