Maiti ya Meles yarudishwa nyumbani | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.08.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maiti ya Meles yarudishwa nyumbani

Maelfu ya raia wa Ethiopia walikusanyika katikati mwa mji mkuu Addis Ababa jana, kuipokea maiti ya waziri mkuu wao, Meles Zenawi, ambaye alifariki katika hospital moja mjini Brussels, Ubelgiji.

Hayati Meles Zenawi aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia

Hayati Meles Zenawi aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia

Kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari na watu kwenye barabara inayotoka uwanja wa ndege wa mjini Addis Ababa kuelekea nyumbani kwa marahemu Meles Zenawi, ambako maiti yake imewekwa ili wananchi waweze kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi wao.

Jeneza lenye mwili wa marehemu ambalo lilifunikwa na bendera ya taifa lilisindikizwa na bendi ya jeshi, huku wakiwepo pia wanasiasa, maafisa wakuu wa jeshi, wanadiplomasia na viongozi wa kidini. Mke wake Azeb Mesfin ambaye alijitandia kwa mavazi meusi ya msiba, aliisindikiza maiti ya mumewe ambayo kutoka Brussels ilisafirishwa na shirika la ndege la Ethiopia. Baadhi ya waombolezaji walibeba picha za Meles.

Mwisho wa minong'ono

Kifo cha waziri mkuu huyo ambacho kilitangazwa usiku wa kuamkia jana, kilimaliza uvumi wa miezi kadhaa kwamba kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 57 alikuwa na matatizo makubwa kiafya. Ethiopia imetangaza kuwa taifa liko katika kipindi cha maombolezo, lakini tarehe ya mazishi bado haijatangazwa.

Hailemariam Desalegn Kaimu Waziri Mkuu wa Ethiopa

Hailemariam Desalegn Kaimu Waziri Mkuu wa Ethiopa

Naibu waziri mkuu Hailemariam Desalegn mwenye umri wa miaka 47, na ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nchi za nje tangu mwaka 2010 ndiye atakayekuwa kiongozi wa mpito, hii ikiwa ni kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Ethiopia, Bereket Simon.

Kulingana na katiba ya Ethiopia, Hailemariam atakula kiapo mbele ya bunge kabla ya kuchukua majumu yake kama kaimu waziri mkuu. Msemaji wa serikali alisema kikao cha bunge kwa ajili ya kiapo hicho kitaitishwa mapema iwezekanavyo.

Maoni yanayokinzana

Chini ya Uongozi wa Meles, Ethiopia ilikuwa na mchango mkubwa kikanda

Chini ya Uongozi wa Meles, Ethiopia ilikuwa na mchango mkubwa kikanda

Wachambuzi wamekuwa na maoni tofauti kuhusu kifo cha Meles Zenawi na athari zake katika siasa za Ethiopia. Ingawa kuna wale wanaochukulia kifo hicho kama kukatiza kasi ya maendeleo makubwa ambayo Meles ameyasimamia wakati wa utawala wake wa miaka 21, kuna pia wale ambao wanaamini kuwa kuondoka kwa Meles ni tukio zuri kwa demokrasia nchini Ethiopia.

Jakkie Cilliers kutoka taasisi ya masomo ya kiusalama iliyoko nchini Afrika Kusini, anadiriki hata kusema kuwa kifo cha Meles Zenawi, kimemuepusha na hali ya kung'ang'ania madaraka na hata mwishowe kuipeleka nchi pabaya.

''Ameondoka kwa wakati unaofaa. Maana yake hatang'ang'ania tena madaraka kama Museveni na Mugabe, hadi kuipeleka nchi kwenye kipindi cha giza. Ni nafasi nzuri kwa Ethiopia.'' Alisema Jakkie Cilliers.

Meles Zenawi anasifiwa kwa kuufufua uchumi wa Ethiopia na kuboresha miundo mbinu, lakini pia anakosolewa na wanaharakati wa kidemokrasia kuitawala nchi kwa mkono wa chuma.

Kifo chake kimeacha pengo kubwa la kiuongozi katika pembe ya Afrika, ambako Ethiopia ilitoa mchango mkubwa katika kuamua mustakabali wa nchi kadhaa zilizo jirani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com