1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahmud Abbas atoa mwito wa kuacha mashambulio

5 Januari 2005

Israel imesema ipo tayari kumruhusu mwenyekiti mpya wa chama cha PLO bwana Mahmud Abbas kuendesha kampeni katika Jerusalem ya msahariki ,sehemu ambayo inakaliwa na Israel tokea mwaka wa 1967

https://p.dw.com/p/CEHA

Bwana Abbas ni mtu mwenye mategemeo makubwa ya kushinda katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii. Hapo awali Israel haikumruhusu hayati Yassir Arafat kuitembelea Jerusalem ya mashariki wakati akiwa mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina. . Wapalestina wanataka Jerusalem ya mashariki uwe mji mkuu wao.

Hatahivyo habari zaidi zinasema kwamba bwana Abbas hataenda kuutembelea msikiti wa Al Aqsa sehemu inayoshika nafasi ya tatu katika uzito wa utakatifu miongoni mwa jamii ya kiislamu duniani.

Msemaji mmoja wa Israel ameeleza kwamba bwana Abbas hatatoa ombi la kuenda kwenye sehemu hiyo takatifu kwa sababu za kiusalama.

Kuna hatari inayotokana na makundi ya wapiganaji wenye siasa kali wanaodhamiwa na Iran.

Waziri Mkuu wa Israel bwana Ariel Sharon ameruhusu wakaazi wa Jerusalem mashariki washiriki katika uchaguzi wa jumapili.

Mjumbe mwingine atakaesimama katika uchaguzi huo wa rais ni bwana Mustafa Barghuti ambaye hivi karibuni alitiwa ndani na idara za usalama za Israel kwa kujaribu kukaa kwa muda mrefu katika Jerusalem ya mashariki.Bwana Barghuti ana ruhusa ya kupitia tu katika mji huo na siyo kukaa.

Wakati huo huo wapalestina wenye siasa kali wamekataa mwito wa bwana Mahmud Abbas juu ya kuacha kufanya mashambulio ya roketi dhidi ya Israel ambapo kituo kimoja cha kijeshi cha Israel kilishambuliwa.

Msemaji wa majeshi ya Israel ameeleza kwamba watu 12 walijeruhiwa katika shambulio hilo karibu na mpaka baina ya Israel na Gaza. Baadhi ya majeruhi hao wamepelekwa hospitali. Wapalestina hao walifanya shambulio jingine la roketi ambalo halikuleta madhara yoyote.

Bwana Abbas amekuwa anajaribu kuwashawishi wapalestina wenye siasa kali kuacha kufanya mashambulio hayo ya roketi na kwamba hayaleti manufaa yoyote.

Jana wapalestina saba ikiwa pamoja na mtoto aliyekuwa na umri wa miaka 11 waliuawa baada ya majeshi ya Israel kuishambulia kwa mizinga nyumba moja kaskani mwa Gaza kujibu mashambulio ya roketi yaliyofanywa na wapalestina wenye siasa kali.

Idadi ya vifo miongoni mwa Wapalestina imeongezeka leo baada ya mtu mmoja aliyekuwa na silaha kupigwa risasi na majeshi ya Israel .

Habari zaidi zinasema kwamba polisi wasiopungua watatu wa kipalestina walijeruhiwa wakati majeshi ya Israel yalipopambana na wapalestina wenye siasa kali waliojipenyeza na kuingia ndani ya mpaka.

Hatahivyo mwito wa bwana Abbas mpaka sasa unaendelea kupuuzwa na wapalestina wengi. Lakini hayo hayataathiri mawezekano ya kushinda katika uchaguzi wa rais siku ya jumapili.Kura za maoni zinaonyesha kwamba bwana Abbas yupo mbele kwa asilimia 30 .

Katika tukio jingine msafara wa mahujaji 400 waliokuwa njiani kwenda Saudi Arabia kutokea Gaza uliambiwa kurudi ulipotokea na majeshi ya Isreal wakati majeshi hayo yalipokuwa yanawasaka wapiganaji wa kipalestina kufuatia tukio la mpakani.Mahujaji alfu nne na mia tano wakipalestina wamepewa vibali vya kwenda kuhiji kwa kupitia Isreal na Misri. Katika msako huo majeshi ya Israel yaligundua bomu

Habari zaidi kutoka Palestina zinasema waziri wa mambo ya nje wa Uturuki bwana Abdullah Gul alitarajiwa kuanza mazungumzo na viongozi wa Palestina juu ya shughuli za ujenzi mpya kwenye ukanda wa Gaza baada ya kuondoka kwa Isreal .

Bwana Gul alitazawamiwa kukutana na waziri mkuu bwana Ahmed Qurei,mawaziri wenzake Nabil Shaath na Saeb Erakat.Mgeni huyo kutoka Uturuki pia anatazamiwa kukutana na bwana Mahmud Abbas.