1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahama mgombea Urais Ghana uchaguzi wa Desemba 2012

27 Julai 2012

Chama tawala cha National Democratic Congress nchini Ghana kimeridhia kumsimamisha Rais wa mpito John Dramani Mahama kuwa mgombea wake kwenye uchaguzi wa mwezi Desemba.

https://p.dw.com/p/15fEz
John Dramani Mahama
John Dramani MahamaPicha: Reuters

Taarifa hiyo inajibu maswali yalikyokuwa vichwani mwa raia juu ya nani atasimama kwenye uchaguzi huo kufuatia kifo cha John Atta Mills.

Halmashauri Kuu ya chama hicho imekubaliana na uamuzi huo wa Mahama kugombea Urais kwa tiketi ya NDC bila pingamizi. Naibu Katibu Mkuu wa NDC George Lawson ameliambia Shirika la Habari la Reuters mara baada ya kikao mjini Accra kuwa tarehe Mosi ya mwezi Septemba baraza kuu la chama litamtangaza rasmi mgombea huyo.

Mahama atachuana na Nana Akufo Addo ambaye aligombea kwenye uchaguzi uliopita na marehemu John Atta Mills. Unatarajiwa kuwa mchuano mkali katika siasa za Ghana.

Nana Akufo-Addo - mgombea wa Ghana atakayechuana na Mahama
Nana Akufo-Addo - mgombea wa Ghana atakayechuana na MahamaPicha: AP

Hapo jana NDC kilimthibitisha Rais Mahama kuwa kiongozi wake katika hatua ambayo ilionekana kuwa ni kuimarisha nafasi yake ya kuwa mgombea wa chama hicho kwenye uchaguzi huo.

Lawson amesema na hapa ninamkunuu " hakukuwa na upinzani wowote kwenye maamuzi hayo", mwisho wa kumnukuu. Wana imani kubwa na Mahama ambaye anaonekana kuthamini kilichofanywa na mtangulizi wake.

Hali ni tofauti na ya marehemu Mills

Mjumbe wa hamashauri kuu ya chama hicho Richard Quashigah amesema kuwa uamuzi huo wa kumpa Mahama fursa ya kuwania kiti cha urais una maana kuwa hakuna mtu mwingine wa kushindana naye chamani. Atakuwa mgombea pekee wa NDC. Hali hii inaondoa mianya ya kuwepo mivutano na mitafaruku ndani ya chama kuhusu nani awe mgombea wakati huu wa kulelekea uchaguzi.

Uamuzi huo ni tofauti na ilivyokuwa kwa mtangulizi wake marehemu Mills. Yeye alichuana vikali na Nana Konadu kupata tiketi ya chama kwenye uchaguzi wa urais uliopita. Konadu ni mke wa aliyekuwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Jerry Lawrings ambaye hadi sasa bado anaushawishi mkubwa kwenye siasa za nchi hiyo.

Marehemu John Atta Mills na Jerry Rawlings, marais wa zamani wa Ghana
Marehemu John Atta Mills na Jerry Rawlings, marais wa zamani wa GhanaPicha: Getty Images

Mchambuzi mmoja nchini humo amesema kuwa hatua hiyo ni maendeleo muhimu kwa chama hicho na kusifu kuwa kimetumia akili sana. Anasema miezi michache tu imesalia kabla ya uchaguzi hivyo chama kitaelekeza juhudi zake kwenye mchakato huo badala ya harakati za kuchagua mgombea. Wanachama wote wa NDC wataungana na kumuunga mkono mgombea wao kwa dhati.

Matarajio ya upinzani kutoka kwa mke wa Rawlings yamepotea

Watu walitaraji kuwa huenda sehemu ya wanachama wangemuunga mkono mke wa Rawlings kuwania tena kupata tiketi ya kugombea. Hali hiyo ilileta shida katika uchaguzi uliopita. Baadhi ya wajumbe wanaamini kuwa nguvu yake kisiasa imepungua.

Wananchi wakimuunga mkono Marehemu Mills uchaguzi uliopita
Wananchi wakimuunga mkono Marehemu Mills uchaguzi uliopitaPicha: AP

Rawlings mwenyewe bado ni mjumbe wa halmashauri kuu ya chama. Hakushiriki maamuzi hayo kwa kuwa alikuwa safarini nje ya nchi ingawa alialikwa.

Mahama, mtaalamu wa masuala ya historia na mwandishi wa vitabu anatarajiwa kwa kiasi kikubwa kufuata nyayo ya mtangulizi wake marehemu Mills wakati huu wa kipindi cha mpito. Amekuwa makamu wa rais wa Mills tangu mwaka 2009 alipochaguliwa.

Mwandishi: Stumai George

Mhariri:Josephat Charo