1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Mahakama yabatilisha bunge Misri

Mahakama ya juu nchini Misri imetangaza kuwa bunge la nchi hiyo ni batili kwa sababu sheria iliyotumika kuandaa uchaguzi wake ilikuwa batili, wakati huo huo ikimsafishia njia Ahmed Shafique kushiriki uchaguzi wa rais.

Ahmed Shafiq

Ahmed Shafiq

Mahakama hiyo imesema sheria iliyotumika kumuwekea vikwazo Shafique ni batili na hivyo ana haki ya kuendelea kugombea kiti hicho ambapo uchaguzi wa duru ya pili utafanyika siku ya Jumamosi na Jumapili, akipambana na mgombea aliyeshika nafasi ya kwanza, Mohammed Mursi kutoka chama cha udugu wa Kiislam.

Hukumu hii inamaanisha kuwa Baraza la kijeshi ambalo limeitawala Misri tangu kuondolea kwa Hosni Mubarak Februari 11 mwaka 2011, litachukua majukumu ya kutunga sheria. Majenerali wa baraza hilo walifanya kikao cha dharura baada ya kutolea hukumu hiyo ambayo inaitia Misri katika mashaka zaidi.

Hatuayataki mamlaka hayo, lakini uamuzi huo wa mahakama na kwa mujibu wa sheria, yanarudi kwetu, kilisema chanzo kimoja kutoka baraza hilo la kijeshi ambalo limeshtumiwa na maafisa wa chama cha Udugu wa Kiislam kula njama za kufanya mapinduzi.

Wandamanaji Mjini Cairo

Wandamanaji Mjini Cairo

Mkanganyiko zaidi
Kiongozi wa mahakama ya katiba, Farouq Sultan aliliambia shirika la habari la AFP kuwa hukumu hiyo imelibatilisha bunge na kwamba mamlaka laazima ziheshimu uamuzi huo. ALifafanua kuwa hukumu inabatilisha bunge na wala sio katika maana ya kulivunja, lakini akaongeza kuwa uamuzi huo wa mahakama ya katiba unahusu mamlaka zote za kitaifa na watu wote.

Mahakama ilitoa hukumu kwa misingi ya vipengele ilivyoviita batili katika sheria ya uchaguzi wa wabunge ambayo inaweka moja ya tatu ya viti kwa wagombea binafsi waliochaguliwa moja kwa moja, au wanachama wa vyama na vingine kwa orodha za vyama.

Utawala wa kijeshi nchini Misri uliamua juu ya mfumo wenye utata ambapo wapiga kura wanachagua wagombea kupitia vyama ambavyo vinachangia mbili ya tatu ya bunge lote na kwa wagombea binafsi kwa ajili viti vilivyosalia. Wagombea moja moja walipaswa kuwa wagombea binafsi, lakini wanachama wa vyama waliruhusiwa kugombea na hivyo kuwapa faida wanaharakati wa Kiislam.

Hukumu dhidi ya Sheria ya Kutengwa Kisiasa
Mahakama pia imeamua kuwa Sheria ya Kutengwa kisiasa inayolenga kuwazuia maafisa wote walioshika nyadhifa za juu katika utawala huo na wale wa chama chake kilichopigwa marufuku cha National Demokratik kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa umma nchini Misri kwa muda wa miaka 10 inakiuka katiba ya nchi.

Mohammed al-Beltagi, mwanachama mwandamizi wa chama cha Uhuru na Haki (FJP) kinachoongoza kwa wingi wa wabunge, aliielezea hukumu hii kama sehemu ya mapinduzi ya kijeshi.

Mgombea wa urais kupitia chama cha udugu wa Kiislam Mohammed Mursi.

Mgombea wa urais kupitia chama cha udugu wa Kiislam Mohammed Mursi.

Alisema hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa katika siku za hivi karibuni, ikiwemo kuruhusu wanajeshi kukamta watu na sasa hukumu hii, ni mapinduzi kamili ambapo Baraza la kijeshi limeyatumia kufuta kipindi cha heshima zaidi katika historia ya Misri, alisema katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari. FJP nayo ilifanya kikao cha siri baada ya hukumu hiyo kujadili hatua inayofuata.

Nje ya mahakama, kiasi ya watu walikusanyika wakidai utekelezaji wa sheria, huku kukiwa na ulinzi mkali. "Ndiyo basi tena! mapinduzi yameisha, alisema mwandamanaji mmoja, huku wengine wakiimba nyimbo dhidi ya utawala wa kijeshi.

Ahmed Shafique, aliyeteuliwa na Mubarak kushika wadhifa wa Waziri Mkuu katika siku za mwisho za utawala wake, aliruhusiwa kugombea urais baada ya tume ya uchaguzi kumruhusu katika dakika za mwisho na licha ya pingamizi kutoka kwa raia wa Misri, alifanikiwa kupenya katika duru ya kwanza baada ya kushika nafasi ya pili na hivyo kuingia duru ya pili ambapo anatarajiwa kuchuana na mgombea wa chama cha Udugu wa Kiislam, Mohammed Mursi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\DPAE
Mhariri: Saum Yusuf