Maoni ya wahariri
11 Machi 2008
Mwenyekiti wa chama cha Social Demokratik, kilichomo katika serikali ya mseto nchini Ujerumani, bwana Kurt Beck anakabiliwa na mgogoro ndani ya chama chake kutokana na msimamo wake juu ya chama cha wakomunisti wa zamani.
Juu ya hayo mhariri wa gazeti la STUTTGARTER anasema katika maoni yake kuwa licha ya kurejea tena kwenye jukwaa la kisiasa baada ya kuugua kwa siku mbili tatu, yeye pamoja na mjumbe wa chama cha SPD aliesimama katika uchaguzi wa jimbo la kati la Ujerumani ,Hesse, Andrea Ypsilanti wamemalizika kisiasa.
Gazeti linasema Kurt Beck na Ypsilanti wametia dosari uadilifu wao kutokana na simamo wao juu ya chama cha mlengo wa kushoto cha wakumunisti wa zamani.
Mhariri anasema ni kweli kwamba baraza kuu la chama cha Social demokratik linamwuunga mkono bwana Beck, lakini kisiasa bado hajapata afuaeni.
Kutokana na msimamo wake juu ya chama hicho cha wakomunisti wa zamani, wanachama wengi wa SPD wanataka kujua chama chao sasa kinaelekea wapi?
Hatahivyo mhariri wa gazati la NORDBAYERISCHE KURIER anasema hata mwenyekiti wa chama anaweza kufanya kosa lakini hana budi akiri kuwa amefanya kosa badala ya kujaribu kubabaisha watu.
Mwenyekiti Beck alikuwa na fursa ya kujirekebisha, lakini amepoteza fursa hiyo na yumkini pia amepoteza fursa ya kugombea ukansela mwaka kesho.
Gazeti la FRANFURTER RUNDSCHAU
linasema, licha ya kinachoonekana kuwa
mgogoro ndani ya chama chake,
mwenyekiti Beck bado anadhibiti hatamu
na ataendelea kukiongoza chama hicho.
Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema kuwa bwana Beck hana njia nyingine ila kuendelea kukiongoza chama chake-sababu ni kwamba katika uongozi wa SPD hakuna mbadala; kwa sasa hakuna tena mtu mwengine wa kushika usukani wa uongozi.Wapinzani wake wa ndani hawana ujasiri wa kumkabili.
Pamoja na hayo Kurt Beck anaungwa mkono na mashina ya chama ,licha ya kosa alilofanya - kuashiria utayarifu wa kushirikiana na chama cha wakomunisti wa zamani.
Mhariri wa gazeti la TRIERISCHEN VOLKSFRUEND anasema bwana Beck ameonesha ukakamavu na roho ngumu katika mgogoro unaomkabili lakini haina maana kwamba haiwezekani kupatikana mtu mbadala katika uongozi wa chama SPD.
Gazeti la LANDESZEITUNG linauliza iwapo ni uhalifu kuvunja ahadi katika siasa?
Mhariri wa gazeti hilo anajijibu mwenyewe kwa kusema hapana, la sivyo wanasiasa wote wangelikuwa wahalifu.
Anasema wakati mwingine ni jambo la lazima kuvunja ahadi,mradi hayo yanafanyika wakati mujarab.