1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko Pakistan

Nina Markgraf13 Agosti 2010

Mafuriko yatarajiwa katika eneo la Jacobabad kusini mwa Pakistan.

https://p.dw.com/p/OmqT
Wakaazi Pakistani wakikimbia mafuriko.Picha: AP

Maelfu ya watu hii leo wameukimbia mji mmoja mkubwa eneo la kusini mwa Pakistan , baada ya maafisa wa usalama  kutoa tahadhari ya kutokea mafuriko, huku waokoaji wakijaribu kufikisha misaada kwa mamilioni ya watu walioathirika nchini humo.

Watu walitumia usafiri wa kila aina ukiwemo wa magari hadi wanyama, kuondoka katika mji huo wa Jacobabad ulio na watu takriban laki 4.

Afisa mratibu  wilayani humo,Kazim Ali Jatoi ameeleza kuwa kuna shinikizo kubwa katika mfereji wa Noorwah na kuna hatari ya maji kutoka kwenye mfereji huo kuvuka matuta yaliyowekwa wakati wowote. Afisa huyo ameeleza kuwa wito umetolewa kwa wakaazi hao kulihama eneo hilo.

Hata hivyo watu wengi wanasita kuondoka kuwacha makaazi na mali zao.

Jacobabad ni mji wa pili mkubwa ambao wakaazi wake wamehamishwa tangu wiki iliyopita, wakati mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kuu za masika zilinyesha, na kuzamisha maelfu ya vijiji na kuathiri zaidi ya watu milioni 16.

Mwanzoni mwa juma hili, watu takriban laki nne na nusu waliuhama kwa uoga mji wa Muzaffargah uliopo katika mkoa wa kati wa Punjab, na kuelekea katika mji mwingine uliopo karibu wa Multan,sehemu ambayo haijaaminika kuwa salama kwa wakaazi dhidi mafuriko hayo.

Pakistan Flut Katastrophe 2010 Flash-Galerie
Mama awabeba watoto wake katika eneo la Muzaffargarh lililoathirika na mafuriko.Picha: AP

Hapo awali maafisa wa usalama walieleza kuwa eneo hilo la Multan linatishiwa na tukio jingine la mafuriko katika mto wa Chenab,  lakini baadaye ikasemekana kuwa maji katika mto huo, yalianza kupungua na ni kiwango kidogo tu kinachotarajiwa kufika katika eneo hilo la Multan.

Uhamisho katika mji huo wa Jacobabad unajiri siku moja baada ya serikali nchini humo kutangaza mipango ya kuimarisha jitihada zake za uokoaji na utoaji misaada kwa waathirika wa mafuriko hayo, yaliyo mabaya zaidi kuwahi kutokea katika miaka 100.

Baada ya kuzuru maeneo yalioathirika na mafuriko hayo hapo jana, waziri mkuu Yousuf Raza Gilani amesema huenda kiwango cha maafa kwa uhai wa watu,mali,mifugo na rasilmali kikawa cha juu zaidi kinyume na makadirio yaliyotolewa awali.

Waziri huyo mkuu alikutana kwa masaa mawili na rais Asif Ali Zardari na baadaye katika taarifa rasmi kutoka kasri la rais, wawili hao walikubaliana kuwa huenda ukahitajika uhamasisho mkubwa wa raslimali, ikiwemo kuweka umuhimu mpya katika bajeti.

Kama mwenyekiti mwenza wa chama tawala cha watu wa Pakistan, katika taarifa hiyo Rais Zardari, alitoa wito pia kwa maafisa wa chama hicho kuchangia kwa kujenga kambi za misaada na kutoa ripoti za jitihada zao.

Taarifa hiyo pia ilielezea kuwa athari za mafuriko hayo ni makubwa zaidi sasa kuliko tukio la Tsunami mnamo mwaka 2004 au tetemeko la ardhi lililotokea nchini humo mwaka 2005.

Kwa mujibu wa shirika linaloshughulikia majanga ya kitaifa nchini humo,katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Khyber Pakhtunkhwa pekee,mafuriko hayo yamesababisha vifo vya watu 1 384, huku wengine zaidi ya 1000 wakijeruhiwa.

Mwandishi:Maryam Dodo Abdalla/DPAE

Mhariri:Josephat Charo