Maelfu wangojea misaada Pakistan
3 Agosti 2010Serikali ya Pakistan inajitahidi kuwasaidia wahanga ambao wengi wao wamepoteza kila kitu. Helikopta ndio njia pekee ya kuwafikia wahanga hao walionasa katika vijiji vilivyozingirwa na maji. Wanajeshi pia wamepelekwa kusaidia, lakini hawatoshi kuhudumia umati wa watu unaongojea misaada ya dharura na wengi wao wanalalamika kuwa serikali wala haijali kama alivzosikitika mama mmoja.
" Mpaka sasa hakuna waziri ye yote yule aliekuja kujua hali zetu. Wanajeshi ndio wanaotusaidia."
Mama huyo si peke yake kulalamika kuhusu wanasiasa wao na kuwa hatua za kuwaokoa na kuwapatia misaada zinakawia. Sasa pia kuna hofu kuwa wanamgambo huenda wakaingilia kati, katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kaskazini-Magharibi.
Mashirika ya misaada kama vile shirika la Umoja wa Mataifa WFP, linaloshughulikia mipango ya chakula duniani, yanajitahidi yawezavyo, kupunguza dhiki za wahanga hao wa mafuriko. Mwenyekiti wa tawi la WFP katika kanda hiyo,Dominique Frankefort anasema kuwa hadi sasa, wameweza kuokoa kama familia 6,000 na juma hili, wanatazamia kusadia familia zingine 35,000. Bado kuna maelfu na maelfu ya watu walionasa katika maeneo ambayo ni shida kufikisha misaada. Wale waliookolewa, wanaishi katika kambi za wakimbizi na wala hawajui jinsi maisha yao yatakavyokuwa katika siku zijazo.
Wakati huo huo, misaada ya kimataifa inamiminika nchini Pakistan. Umoja wa Ulaya, Marekani na Umoja wa Mataifa zimeahaidi mamilioni na mashirika ya misaada yametoa mwito kwa wafadhili kutoa michango zaidi. Vile vile, kuna hatari kubwa ya magonjwa ya kuambukizana kuripuka. Ama hakuna kabisa maji ya kunywa au yaliyokuwepo ni machafu.
Kama mchambuzi mmoja alivyoeleza: hivi sasa, Pakistan haikabiliwi tu na maadui Taliban bali inapambana na maafa ya kimaumbile vile vile. Mara nyingine tena kumezuka suala iwapo Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari kweli amejizatiti na ana uwezo wa kutenzua matatizo yanayoikabili nchi hiyo na iwapo hatimae ataweza kuleta hali ya utulivu nchini humo.
Mwandishi:Küstner,Kai/ZPR/P.Martin
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman