1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana tena huko Belarus dhidi ya Lukashenko

Sylvia Mwehozi
6 Septemba 2020

Maelfu ya raia wa Belarus wameandamana Jumapili na kuzidisha shinikizo dhidi ya kiongozi mwenye nguvu  Alexander Lukashenko ambaye amekataa kuondoka madarakani baada ya uchaguzi uliompatia ushindi kuibua utata.

https://p.dw.com/p/3i4tu
Proteste in Belarus
Picha: picture-alliance/dpa/AP

Maafisa wa usalama waliojihami na magari ya maji ya kuwasha walisambazwa katikati mwa Minsk kuelekea maandamano ya Jumapili huku stesheni kadhaa za treni za chini ya ardhi zikifungwa

Lakini waandamanaji wa kila rika, kuanzia wazazi, watoto, wanafunzi, mapadri wa Kikatoliki na wanariadha mashuhuri walimiminika mitaani ikiashiria kukiuka onyo la kutoandamana.

Maandamano hayo yasiyo ya kawaida yalizuka baada ya Lukashenko aliyeitawala Belarus kwa miaka 26, kudai kuwa amechaguliwa tena kwa asilimia 80 katika uchaguzi uliofanyika Agosti 9.

Kiongozi wa upinzani  Svetlana Tikhanovskaya anadai kuwa yeye ndio alishinda uchaguzi. Maafisa wa usalama wamewakamata maelfu ya waandamanaji, wengi wakiwatuhumu polisi kwa kuwapiga na kuwatesa. Watu kadhaa wamepoteza maisha katika ukandamizaji huo. Tikhanovskaya aliondoka Belarus na kutimkia Lithuania nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Wiki ijayo, kiongozi huyo atasafiri kuelekea mjini Warsaw Poland kama alivyonukuliwa katika ujumbe wake kwa njia ya vidio akisema ari ya waandamanaji kwa hivi sasa haiwezi kubadilishwa. "Wabelarus tayari wamebadilika, wameamka na ni vigumu kuwarejesha nyuma katika fikra za zamani", alisema kiongozi huyo.

Weißrussland | Proteste in Minsk
Maafisa wa usalama wakiwa tayari kuwakabili waandamanaji mjini MinskPicha: DW/P. Bykouski

Kundi la haki za binadamu la Spring-96 limedai kuwa takribani watu 70 wamekamatwa. Shirika la habari la Urusi Interfax limeripoti kwamba watu kadhaa wamejeruhiwa wakati polisi walipotawanya umati wa waandamanaji nje ya kiwanda cha utengenezaji matrekta.

Wizara ya mambo ya ndani katika taarifa yake imesema kwamba waandamanaji 91 walikamatwa siku ya Jumamosi, na kwamba itazidisha usalama na kuchukua hatua zote zinazohitajika kuzuia vurugu na kuvurugwa kwa amani. Katika mahojiano yaliyochapishwa na Financial Times Jumapili, waziri wa mambo ya kigeni wa Lithuania Linas Linkevicius ameutolea mwito Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo Belarus na kukabiliana na ushawishi wa Urusi. Soma Waandamanaji waongeza shinikizo kwa rais Lukashenko

"Wakati mwingine tunachelewa kuchukua hatua na hatua zetu zimegawanyika na hazitoi maana kwa jamii na viongozi walioko madarakani". Luthuania, Latvia na Estonia zimetoa zuio la kusafiri kwa Lukashenko na maafisa wengine 29 wa Belarus bila ya kusubiri nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kukubaliana juu ya hilo.

Wabelarus wamekuwa wakiandamana kwa takribani mwezi mmoja, licha ya kwamba maandamano hayo yanakosa kiongozi wa wazi, ambapo wanaharakati wengi wamefungwa au kulazimika kukimbia nchi. Zaidi ya watu 100,000 wamekuwa wakifurika katika mitaa ya mji mkuu wa Minsk na maandamano ya Jumapili yanasemekana kuwa makubwa zaidi.