Mada moja tuu imehanikiza magazetini hii leo | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 21.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mada moja tuu imehanikiza magazetini hii leo

Ripoti ya mwaka kuhusu hali namna ilivyo katika jeshi la shirikisho Bundeswehr

Ripoti ya mjumbe wa bunge la shirikisho Bundestag aliyepewa jukumu la kutathmini hali ya mambo ndani ya jeshi la shirikisho Bundeswehr imeshughulikiwa kwa mapana na marefu na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Ripoti hiyo iliyochapishwa na mjumbe maalum wa bunge la shirikisho REINHOLD ROBBE inazungumzia juu ya ukosefu wa fedha na kupuuzwa huduma za afya na huduma nyenginezo katika kambi za jeshi la shirikisho kutokana na majukumu yake nchi za nje.

Gazeti la ALLGEMEINE ZEITUNG la mjini Mainz linaandika:

„Ujerumani inataka kubeba jukumu kubwa kabisa katika siasa za kimataifa.Inamaanisha kwa hivyo jeshi la shirikisho Bundeswehr liwajibike nje kabisa ya nyumbani.Ripoti ya mjumbe maalum wa bunge la shirikisho inamfanya mtu aamini kwa bahati mbaya kwamba mwanya kati ya matakwa na uwezo ni mpana na huo ndio ujumbe halisi kwa serikali ya muungano mjini Berlin.Jeshi la shirikisho halijajiandaa vya kutosha na wala halina zana za kutosha kuweza kukabiliana na majukumu mepya.Ndio maana orodha hiyo yenye kasoro iliyoandaliwa na mjumbe maalum wa bunge la shirikisho haistahili kufungiwa kabatini,badala yake itumike kama msingi wa kulifanyia mageuzi ya kina jeshi la shirikisho Bundeswehr.“

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG la mjini München linaamini:

„Jeshi la shirikisho halina wakuwapigania.Nafasi za kuwalea watoto wadogo na shule za chekechea tuu ndizo mada zinazohanikiza.Bundeswehr inaingia midomoni tuu pakizuka kashfa au mjumbe maalum anapochapisha ripoti yake ya mwaka.Hata uamuzi wa kutumwa madege ya kivita chapa Tornado nchini Afghanistan haukumshughulisha yeyote mwengine aliyeko nje ya jiji la Berlin.“

Mhariri wa gazeti la LÜBECKER ZEITUNG ameandika:

„Fedha zaidi zingesaidia kutengeneza kambi za kijeshi zilizooza.Fedha zaidi ili kuweza kulingana na sura inayopewa jeshi katika siasa ya nje ya Ujerumani-hata kama serikali haipendelei sana kuzungumzia hali hiyo.Tunasubiri kwa hamu kusikia serikali ya muungano wa vyama vya rangi nyeusi na nyekundu italishughulikia vipi suala hili.“

Gazeti la MAIN-ECHO la mjini ASCHAFFENBURG linaandika:

“Wanasiasa hawataweza tena kuifumbia macho hali mbaya kama hiyo hasa kwasababu inadhoofisha nguvu za jeshi na kuyatia hatarini maisha ya wanajeshi.Bunge la shirikisho linawajibika kuhakikisha jeshi la shirikisho Bundeswehr lina zana zote zinazohitajika kuweza kutekeleza ipasavyo majukumu yake kama mshirika wa kuaminika.Hakuna tena kuvuta wakati.Ripoti ya mwaka ya mjumbe maalum wa bunge la shirikisho Bundestag ni onyo.Pasizuke yeyote baadae atakaedai hakua akijua.“

Gazeti la General Anzeiger la mjini Bonn linaandika:

„Ni nadra kumuona mjumbe wa bunge akiwagutua namna hii viongozi wa kijeshi,wabunge na jamii kwa jumla jinsi jeshi la shirikisho Bundeswehr,japo kama sio lote,linavyojikuta katika hali isiyokubalika.Yeyote anaetaka kuwatumia wanajeshi kwa masilaha ya kisiasa,anabidi pia awashughulikie ipasavyo.Katika jeshi la shirikisho sauti zimekua zikipazwa tangu muda mrefu sasa.Jeshi la shirikisho sio tuu halina wanajeshi wa kutosha ,hata zana zimekua haba hivi sasa.“

 • Tarehe 21.03.2007
 • Mwandishi zusammesst:Kümmerling / Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB59
 • Tarehe 21.03.2007
 • Mwandishi zusammesst:Kümmerling / Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB59

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com