1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na shambulio la Bundu Dia Kongo Magazetini

Oumilkheir Hamidou
19 Mei 2017

Matumaini ya nchi za Afrika, baada ya Emmanuel Macron kuchaguliwa kuwa rais wa Ufaransa, kisa cha kuvamiwa jela katika jamhuri ya Kongo na lawama dhidi ya benki ya Ujerumani Deutsche Bank ni miongoni mwa mada Magazetini

https://p.dw.com/p/2dE9i
Frankreich Emmanuel Macron Amtseinführung
Picha: Getty Images/AFP/F. Mori

Tunaanzia njia panda inayoiunganisha Ufaransa na mataifa ya Afrika yanayozungumza kifaransa au Francophonie kama yanavyoitwa."Macron anavutiwa na Afrika" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Neues Deutschland linalosimulia jinsi vyombo vya habari na wakaazi wa nchi hizo za kiafrika zinazozungumza kifaransa walivyofuatilizia kwa makini kuchaguliwa rais huyo kijana. Hata hivyo matarajio yao kwa Emmanuel Macron  yana kikomo miaka 60 tangu nchi hizo zilipojipatia uhuru, linaandika gazeti la Neues Deutschland linalomnukuu  mwanafalsafa, mtaalam wa historia na msomi wa kutoka Kamerun , Professor Aehille Mbembe, anaesomesha katika chuo kikuu cha Witwatersrand cha Afrika Kusini akisema "anaotea siku ambayo waafrika watafuatilizia kwa makini uchaguzi nchini Ujerumani au Marekani kama wanavyofanya kwa Ufaransa. Watarajie nini Waafrika kutoka kwa rais mpya wa Ufaransa Macron linajiuliza gazeti la Neues Deutschland linalomaliza ripoti yake kwa kukumbusha mahojiano aliyokuwa nayo na jarida la Jeune Afrique kabla ya kuchaguliwa kuwa rais na yale aliyoyasema alipotuwa kwa muda nchini Algeria na kuutaja ukoloni kuwa "uhalifu dhidi ya ubinaadam. Katika mahojiano na jarida la Jeune Afrique Emmanuel Macron alitaja utulivu wa kisiasa na amani kuwa mhimili wa siasa yake kuelekea Afrika.

 Kwanini waasi wa Bundu Dia Kongo wameivamia jela ya Malaka

Jamhuri ya kidemkrasi ya Kongo imegonga pia vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani wiki hii. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeandika kuhusu "uasi wa wakaazi wa mashambani dhidi ya marais wenye nguvu. Kwa jumla gazeti hilo linazungumzia kisa cha kuvamiwa jela kuu ya Malaka na kundi la watu 100 waliokuwa na silaha na kumtorosha kiongozi wa kundi la kidni lililopigwa marufuku  nchini humo Bundu Dia Kongo, Ne Muanda Nsemi na wafuasi wengine 50 wa kundi hilo ambalo tafsiri yake kwa kiswahili ni Ufalme wa Kongo. Baada ya kukumbusha  Nsemi  ni nani, mbunge aliyekamatwa mwezi March kutokana na miito yake ya kila mara kutaka watu wasiwatii wawakilishi wa serikali, Frankfurter Allgemeine linasema shambulio dhidi ya jela ya Malaka halijatokea bure mnamo siku ya kuadhimisha miaka 20 tangu alipong'atuka Mobutu Sese Seko. Gazeti linamaliza kwa kuandika "mtu hahitaji kuwa mpiga ramli kuweza kuashiria malumbanao ya umwagaji damu yanayoweza kuutikisa mkoa wa kati wa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo wiki zinazokuja."

Deutsche Bank inatakiwa isiyakopeshe makampuni yasiyoheshimu haki za binaadamu Afrika

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa wa Afrika katika magzeti ya Ujerumani wiki hii inaturejesha hapa hapa nchini Ujerumani ambako gazeti la mjini Berlin, die Tageszeitung linaripoti kuhusu tuhuma za shirika lisilomilikiwa na serikali dhidi ya benki mashuhuri ya Ujerumani Deutsche Bank kwa kile kinachosemekana kuwa mtindo wenye utata wa kutoa mikopo. Gazeti linazungumzia mkutano wa wadau ulioitishwa alkhamisi iliyopita mjini Berlin ambapo mashirika yanayopigania haki za binaadam Misereor na Facing Finance yameitaka Deutsche Bank isilipatie tena mikopo kampuni la kuchimba migodi la Uswisi Glencore. Kampuni hilo linatuhumiwa kukiuka mwongozo wa kijamii na kimazingira katika nchi kadhaa za Afrika. Deutsche Bank ilikubali hapo awali kulipatia kampuni hilo  mkopo wa Euro bilioni 1.2. Die Tageszeitung limenukuu ripoti inayozungumzia utafiti uliofanywa na kudhihirika kwamba, kampuni hilo la wachimba migodi limehusika na visa vya rushwa na kuziendeya kinyume haki za binaadam katika nchi kadhaa za dunia ikiwa ni pamoja na jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/presse

Mhariri: Mohammed Khelef