1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron: Marekani ilikosea katika mkataba wa nyuklia

10 Mei 2018

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameutaja uamuzi wa Marekani kujiondoa kutoka kwenye mkataba wa nyuklia wa Iran kuwa makosa. Katika mahojiano na DW rais huyo wa Ufaransa amesema Ulaya inastahili kushikilia dhamira yake.

https://p.dw.com/p/2xUAQ
Karlspreis 2018 zu Aachen | Emmanuel Macron, Präsident Frankreich | DW-Interview
Picha: DW/B. Riegert

Mkataba huo uliotiwa saini mwaka 2015 kuhakikisha kwamba Iran haianzi tena harakati zake za nyuklia na kuzuia taharuki katika eneo la Mashariki ya Kati.

Macron amesema kwamba alifahamu awali katika ziara yake Marekani kwamba Rais Trump anataka kujiondoa kutoka kwenye mkataba huo, hatua ambayo anaitaja kuwa ni makosa kwasababu ni mkataba unaotoa nafasi ya kudhibitiwa kwa ulinzi wa nyuklia wa Iran hadi mwaka 2025.

"Pendekezo nililoliwasilisha kwa Rais Trump nilipokuwa Washington ni kwamba, "usiharibu kila kitu, iwapo una mashaka kuhusu Iran wacha tuutilie mkazo huu mkataba." Nafikiri mkataba huu unastahili kukamilishwa," alisema Macron.

Uhusiano wa kibiashara wa Kanda ya Atlantiki haujaharibika

Kujiondoa kwa Marekani katika mkataba huo ni pigo kwani ni mmojawapo wa washirika wakuu katika mkataba huo lakini Macron anasema makubaliano hayo bado yana umuhimu na kwamba kama Ulaya wamewapa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya na Iran jukumu la kuhakikisha kwamba umuhimu wao wa kutojiondoa unaonekana.

Karlspreis 2018 zu Aachen | Emmanuel Macron, Präsident Frankreich | DW-Interview
Rais Macron katika mahojiano na DW na kituo cha Ujerumani cha ARDPicha: DW/B. Riegert

Kuhusu uhusiano wa kibiashara wa kanda ya Atlantiki, Macron amesema bado haujaharibika na kuna uelewano mzuri baina ya Ulaya na Marekani ingawa amekiri kwamba kuna taharuki kwa kiasi fulani. Kulingana na rais huyo Ulaya ni nguvu kubwa ya kibiashara na ingawa Marekani ni mshirika wao, watasalia kufuata sheria za Shirika la Biashara Duniani WTO.

Kuhusiana na masuala ya Ulaya Macron hivi majuzi aliweka wazi ajenda yake ya mabadiliko anayotaka yafanywe katika Umoja wa Ulaya ingawa Ujerumani haijaonyesha kuyaunga mkono. Kuhusiana na hilo rais huyo amesema hajavunjwa moyo na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwani ana matumaini kwamba Ujerumani itakapotoa jibu lake kuhusiana na mapendekezo yake mwezi Juni, litakuwa jawabu zuri.

Amesema anatumai kwamba Merkel na serikali yake wataungana na Ufaransa katika kufanya kazi pamoja kwa ajili ya Ulaya yenye nguvu na demokrasia kwakuwa sasa hiyo ndiyo changamoto kuu.

Macron apewa tuzo ya Charlemagne kwa kutoa "Dira ya Ulaya"

Mojawapo ya mapendekezo aliyokuwa ameyatoa Macron katika suala la mageuzi ndani ya Umoja wa Ulaya ni kubuniwa kwa nafasi ya Waziri wa Fedha wa Umoja wa Ulaya jambo ambalo halipokelewi vyema Ujerumani ila Macron anasema hatarajii yote aliyopendekeza kutekelezwa. Kwani anahisi lilikuwa ni jukumu lake kutoa mapendekezo kutokana na dhamira aliyokuwa nayo.

Verleihung Internationaler Karlspreis an Macron
Macron akipokea tuzo ya Charlemagne mjini AachenPicha: Reuters/W. Rattay

Rais huyo wa Ufaransa amepewa tuzo ya Charlemagne kwa hatua yake ya kutoa "Dira ya Ulaya Mpya" ambapo ameyataka mataifa ya Ulaya kufanya juhudi zaidi kuhakikisha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana unapungua.

Amepokea tuzo hiyo ambayo imekuwa ikitolewa kila mwaka tangu mwaka 1950 katika sherehe itakayoandaliwa katika mji wa Aachen. Aachen ndiyo yaliyokuwa makao ya Charlemagne ambaye anajulikana kama "baba wa Ulaya" ambaye alifanikiwa kuileta pamoja Ulaya Magharibi katika karne ya tisa.

Mwandishi: Jacob Safari/DW

Mhariri: Iddi Ssessanga