1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabingwa wa zamani wa Ulaya Dernmark wang´olewa katika michuano ya Kombe la dunia

25 Juni 2010

Kiungo wa Japan Keisure Honda,arithi mikoba ya Hidetoshi Nakata

https://p.dw.com/p/O2rf
Kiungo wa kutumainiwa wa Japan katika michuano ya kombe la dunia,Keisuke Honda akishangilia baada ya kufunga goli.Picha: AP

Maajabu yanazidi kujitokeza katika michuano ya mwaka huu ya kombe la dunia,baada ya hapo jana kung´olewa kwa mabingwa wa soka Itali na timu isiyotarajiwa ya Slovakia,lakini pia timu mbili kutoka bara la Asia za Korea kusini na Japan kufaulu kuingia duru la pili.

Mshambuliaji ambaye kwa sasa anagonga vichwa vya habari ulimwenguni kutoka Japan,Keisure Honda, anabashiriwa kuwika zaidi mwaka huu,na kuwafunika nyota wa kulipwa barani Ulaya,wakiwemo Wayne Rooney na Ricardo Kaka,ni maajabu gani yatatokea tena katika michuano hii?

Hili ndilo swali ambalo wafuatiliaji wa soka ulimwenguni wanajiuliza.

Keisuke Honda mfungaji wa bao lililoizamisha Cameroon katika mechi ya ufunguzi ya kombe la dunia,amedhihirisha tena kuwa hakubahatisha,kwani hapo jana ndiye aliyekuwa chachu ya ushindi wa kushangaza wa mabao 3 -1 dhidi ya Denmark na kuwafungisha virago mabingwa hao wa zamani wa Ulaya katika michuano ya mwaka huu.

Mchezaji huyo nyota yake ilizidi kung´ara baada ya kufunga bao moja na kutengeneza lingine moja katika ushindi mnono ilioupata dhidi ya Dernmark,na kuanza kulitangaza soka la ushindani la bara la Asia,kufuatia timu nyingine kutoka bara hilo,Korea kusini nao kufanikiwa kuingia duru ya pili ya mtoano.

Kocha aliyemuibua kiungo huyo na kumfunza soka la kulipwa akiwa shuleni,Mamori Kawasaki, ameeleza baada ya mchezo huo kwamba Honda,alionekana tangu mwanzo wa michuano hii,kuwa na malengo ya kulitangaza soka lake,hivyo amethibitisha kuwa mchezaji huyo ni nyota mpya ya soka la Asia,baada ya kiungo Hidetoshi Nakata ambaye kwa sasa amestaafu soka la kulipwa.

Naye Hidetoshi Nakata aliyeamua kustaafu soka la kulipwa baada ya Japan kung´olewa katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2006 hapa Ujerumani,amekisifu kikosi hicho na kueleza kuwa kimeonekana kuimarika zaidi mwaka huu,na kuwataka kuongeza bidii ili kuvuka mafanikio ya mwaka 2002.

Ushindi wa Japan pia umepokelewa kwa furaha kubwa na Waziri mkuu wa Japan, Naoto Kan, ambaye anahudhuria mkutano wa kimataifa jijini Toronto,Canada,amewapongeza wachezaji wa Japan kwa ushindi huo ambao ameuelezea kuwa ni sifa kwa soka la Japan.

Kutokana na ushindi huo,Japan itakumbana na Paraguay katika hatua ya mtoano siku ya jumanne,ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo tangu mwaka 2002 ilipoandaa michuano hiyo kwa ushirikiano na Korea kusini.

Katika hatua nyingine,timu pekee kutoka Afrika, Ghana inatajwa kuwa huenda ikarejea historia ya mwaka 2006 katika michuano ya kombe la dunia,ilipofanikiwa kuiondoa mashindanoni Marekani kwa kuifunga mabao 2 - 1 ,lakini Rais mstaafu wa Marekani Bill Clinton ameeleza kuwa timu yake inaweza kuushangaza ulimwengu kwa kuiwezesha timu hiyo kuvuka hatua ya nusu fainali.

Nahodha wa Marekani,Carlos Bocanegra, ameeleza kuwa haitakuwa kazi nyepesi kuifunga Ghana,huku akielezea ugumu atakaokumbana nao kumkabili mshambuliaji hatari wa Ghana,Asamoah Gyan mwenye mabao mawili katika michuano ya mwaka huu.

Mpaka sasa mchezaji wa Argentina,Gonzalo Higuain na mchezaji Robert Vittek wa Slovakia wanafukuzana katika kuwania kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora,kutokana na wote kupachika mabao 3 kila mmoja.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/ DPAE/AFPE/RTRE

Mhariri: Miraji Othman