1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabaki zaidi ya AirAsia yagunduliwa

3 Januari 2015

Timu zenye kutafuta mabaki ya ndege ya abiria ya shirika la AirAsia ilioanguka ikiwa na watu 162 zimegunduwa vipande vinne vikubwa vya ndege hiyo chini ya habari.

https://p.dw.com/p/1EEcp
Mwanajeshi wa kikosi cha anga cha Indonesia akiwa kwenye helikopta kutafuta miili na mabaki ya ndege ya AirAsia.
Mwanajeshi wa kikosi cha anga cha Indonesia akiwa kwenye helikopta kutafuta miili na mabaki ya ndege ya AirAsia.Picha: Reuters/Bagus Indahono

Mkuu wa shirika la msako na uokozi la Indonesia Fransiskus Bambang Soelistyo amewaambia waandishi wa habari mjini Jakarta Jumamosi (03.01.2014) kwamba wamegunduwa vipande vinne vikubwa vya mabaki ya ndege hiyo ambayo wamekuwa wakiitafuta.

Ugunduzi huo umekuja wakati serikali ikisema kwamba shirika la ndege la AirAsia limekiuka masharti ya leseni yake ya kutumia njia ya Surabaya kwenda Singapore hapo Jumapili siku ambayo ndege yake hiyo aina ya Airbus A320-200 ilipoanguka kwenye bahari ya Java na kutangaza kwamba watachunguza ratiba nyengine za safari ya ndege za shirika hilo.

Kipande kimoja kikubwa kiligunduliwa na meli iliokuwa ikifanya msako wakati wa usiku na vipande vyengine vitatu zaidi ambacho kikukwa kabisa kikiwa na urefu wa mita 18 vimegunduliwa Jumamosi kwa mujibu wa Solelistyo.

Hali mbaya ya hewa yatatiza

Afisa mwengine wa timu hiyo ya uokozi Supriyadi ambaye anaratibu operesheni za uokozi kutoka bandari ya Pangkalan Bun ilioko Borneo amesema hapo awali kwamba hali ya kutoweza kuona vizuri imekwamisha juhudi za kunasa taswira za vipande hivyo kwa kutumia vyombo vya kuzamia chini ya bahari.

Mtaalamu wa utabiri wa hali ya hewa Indonesia.
Mtaalamu wa utabiri wa hali ya hewa Indonesia.Picha: imago/Xinhua

Amesema uwezo wa kuona unakuwa wa umbali wa mita mbili tu na kwamba kuna mawingu jambo linalofanya iwe vigumu kwa kamera kugunduwa kitu.

Wapiga mbizi ikiwemo timu ya wataalamu ya Urusi ambao ndio kwanza wamewasili huko Pankalan Bun wanaweza kuanza kuchunguza mabaki hayo hapo Jumapili iwapo hali ya hewa itakuwa nzuri.

Hakuna manusura

Hakuna manusura waliogundulika kutokana na ajali hiyo ambayo imetokea kama dakika 40 baada ya ndege hiyo kuruka kutoka Surabaya mji wa pili kwa ukubwa nchini Indonesia katika eneo ambalo linafahamika kwa kuwa na vimbunga vikali hususan wakati huu wa msimu wa mvua.

Ndugu wakiomboleza vifo vya wahanga wa ajali ya ndege ya Air Asia.
Ndugu wakiomboleza vifo vya wahanga wa ajali ya ndege ya Air Asia.Picha: Reuters/Beawiharta

Repoti kutoka katika ofisi ya utabiri wa hali ya hewa nchini Indonesia imesema yumkini ndege hiyo imeruka kwenye hali mbaya ya hewa jambo ambalo ingelikuwa vigumu kuliepuka na kwamba inawezekana hali hiyo imesababisha kuganda kwa barafu kwenye engine za ndege hiyo.

Ofisi hiyo imesema kwa kuzingatia data zilizopatikana mara ya mwisho juu ya mahala iliokuweko ndege hiyo hali ya hewa imesababisha ajali hiyo.

Leseni ya AirAsia yumkini kufutwa

Maafisa wa serikali ya Indonesia hapo Ijumaa walihoji iwapo rubani wa ndege hiyo alifuata taratibu sahihi za hali ya hewa na baadae ikazisitisha safari za shirika hilo la AirAsia za kutoka Surabaya kwenda Singapore kwa kusema kwamba leseni ya safari zake hizo inaziruhusu tu kusafairi siku za Jumatatu,Jumanne, Alhamisi na Jumamosi.

Ndege ya shirika la ndege la AirAsia chapa Airbus 320-200 mfano wa ile iliyopata ajali.
Ndege ya shirika la ndege la AirAsia chapa Airbus 320-200 mfano wa ile iliyopata ajali.Picha: imago/Xinhua

Djoko Murdjatmondo kaimu mkurugenzi mkuu wa Usafiri wa Anga nchini Indonesia amesema hapo Jumamosi kwamba Wizara ya Uchukuzi itachunguza njia nyengine za safari zinazotumiwa na ndege za shirika hilo ambayo husafiri katika vituo 15 nchini Indonesia.

Amesema watachunguza ratiba za safari zote za ndege za shirika hilo la AirAsia na kwamba wanataraji kuanza kufanya hivyo hapo Jumatatu. Ameongeza kusema inawezekana leseni ya shirika hilo la AirAsia nchini Indonesia ikafutwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa

Mhariri: Sudi Mnette